Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenister Mhagama ametoa tahadhali kwa wananchi huhusu utabiri wa uwepo wa mvua za Elnino zinazotabiriwa kutokea msimu huu katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza katika maonesho ya Maafa yanayoendelea Mkoani Manyara Mhagama amezitaka Taasisi zote zinazohusiana na masuala ya Maafa hususan Majanga ya Asili kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi.
Aidha, Waziri Mhagama amewapongeza washiriki wote waliojitokeza kwenye maonesho hayo na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Manyara kutumia fursa zilizopo ili kujifunza na kupata uelewa wa majanga ya asili na namna ya kuepuka madhara ya majanga hayo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako ametumia fursa hiyo kuwataka Vijana wote nchini kuchukua tahadhali ya Majanga ya Asili hususan janga la mvua za Elnino zinazotabiriwa kutokea msimu huu katika maeneo mbalimbali nchini.
Naye, Meneja wa Sehemu ya Mapping Economic Geology na Mkuu wa Kitengo cha Majanga ya Asili Gabriel Mbogoni amesema Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imejipanga kikamilifu kutoa taarifa kwa wakati kuhusu matetemeko ya ardhi yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Wataalumu wa GST wameendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za majanga ya asili na namna ya kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na majanga hayo.