Breaking

Thursday, 19 October 2023

WATANZANIA CHANGAMKIENI FURSA YA KUTATUA CHANGAMOTO ZA KIBIASHARA KATI YA TANZANIA NA MAREKANI

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa rai kwa Sekta Binafsi kutumia fursa ya makubaliano ya majadiliano ya kibiashara kati ya Tanzania na Marekani kubainisha changamoto wanazokumbana nazo wakati wa kufanya biashara na Marekani ili zitatuliwe na kukuza biashara na kuongeza mapato ya wananchi na Taifa.

Aidha, amewakaribisha wafanyabiashara kutoka Marekani kuja Tanzania kufanya biashara na kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa ambazo zitauzwa nchini na kwenye masoko ya EAC, SADC na AfCFTA.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo 10/19/2023 wakati wa hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano ya Majadiliano ya Kibiashara kati ya Tanzania na Marekani (MoU) yaliyofanyika katika ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam.

Pia, Dkt Kijaji amebainisha kuwa Makubaliano hayo yanatarajia kukuza biashara baina ya Tanzania na Marekani hususani uuzaji wa bidhaa kupitia Mpango wa AGOA ambapo mwaka 2022 mauzo ya Tanzania kwenda Marekani yalikuwa na thamani ya Dola Marekani Milioni 74.5 na manunuzi yalikuwa na thamani ya Dola za Marekani Milioni 93.7.

Aidha. Dkt Kijaji ametaja maeneo ambayo yataanza katika majadiiano hayo kutokana na umuhimu wake ambayo ni Uchumi wa Kidigitali (Digital Economy), Upatikanaji wa Masoko (Market Access), Mifumo ya Kisheria na Mazingira ya biashara (Regulatory and Business Environment Reform), ushirikiano kwenye Maonesho ya Biashara (Trade Mission). Mengine yataongezwa kulingana na pande zote mbili

Vile vile amebainisha kuwa hatua ya makubaliano hayo ni mwendelezo wa Jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kufungua fursa za biashara na uwekezaji na nchi mbalimbali duniani. MoU hiyo itasaidia katika kuendeleza na kuimarisha uhusiano wa biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Marekani.

Aidha Dkt Kijaji ameahidi kuendeleza ushirikiano na Waziri wa Biashara wa Marekani Mhe. Gina Raimondo katika kuhakikisha kuwa biashara baina ya Tanzania na Marekani inaendelea kukua na kuimarika.

Naye Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. Michael Battle amesema kupitia makubaliano hayo wafanyabiashara wa Marekani na Tanzania watakuwa wakikutana mara kwa mara hali ambayo itaiwezesha sekta binafsi kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina Tanzania na Marekani.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) (Kulia) akiwa na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Mhe. Michael Battle (kushoto), wakisaini Hati ya Makubaliano ya Majadiliano ya Kibiashara kati ya Marekani na Tanzania Oktoba 19,2023, JNICC, Dar es salaam. Walioko Nyuma ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Leodegar Tenga(kulia), Afisa Biashara Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Bi. Sekela Mwaisela na Afisa Biashara Mwandmizi wa Ubalozi Marekani nchini Bi Aliza Totayo wakishuhudia , hafla iliyofanyika Oktoba 19,2023, JNICC , Dar es salaam
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages