Breaking

Sunday, 15 October 2023

WANAFUNZI JK NYERERE WAISHUKURU BARRICK KWA KUWA MDAU MKUBWA WA KULETA MAPINDUZI KATIKA SEKTA YA ELIMU NCHINI

Sehemu ya wanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari JK Nyerere iliyopo Tarime iliyojengwa na Barrick North Mara wakicheza na kuimba kwa furaha wakati wa mahafali yao shuleni.


Pia wahamasisha jamii kuacha vitendo vya uvamizi wa Mgodi wa Barrick North Mara

***
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Julius Kambarage Nyerere, iliyopo kijiji cha Nyamwaga wilayani Tarime, wameushukuru Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kwa kuwajengea shule hiyo ambayo inachukua wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita wanaosoma masomo ya michepuo mbalimbali.

Aidha, wameishukuru Kampuni ya Barrick inayoendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals, kwa jinsi ambavyo imeendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya shule hiyo sambamba na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha sekta ya elimu nchini.Katika kudumisha ubia na Serikali karibuni Barrick imetoa dola milioni 40 kwenye mpango wa ujenzi wa barabara na dola milioni 30 zaidi katika uboreshaji wa suhula za elimu ya juu nchini.

Walitoa shukrani hizo kupitia risala yao wakati Mahafali ya Saba ya Kidato cha Nne ya shule hiyo iliyofanyika shuleni hapo na kuhudhuriwa na viongozi mbambali wa kijamii, na Serikali akiwemo Diwani wa Kata ya Nyamwaga, Mwita Marwa Magige.

“Tunatoa shukrani za dhati kwa Mgodi wa Barrick North Mara kwani wamekuwa wadau wakubwa wa shule yetu, pia jitihada zinazofanywa na kampuni kuunga mkono Serikali kuboresha sekta ya elimu kupitia kuimarisha miundombinu ya shule na vifaa vya kufundishia kwa lengo la kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kupata elimu bora,” walisema katika sehemu ya risala yao wakati wa hafla hiyo.



Walifafanua katika risala hiyo kuwa mgodi wa Barrick North Mara uligharimia ujenzi wa shule hiyo mwaka 2014, ambapo mwaka 2017 ilitoa wahitimu wa kwanza wa kidato cha nne.

Wanafunzi hao waliongeza kuwa baadaye shule hiyo ambayo imepewa jina la Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilisajiliwa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita, ambapo mpaka sasa imepokea wa kidato cha tano wa awamu ya nne.


“Tunashukuru Mungu kwamba wanafunzi wote waliomaliza kidato cha sita katika shule yetu mwaka huu walifaulu na kuchaguliwa kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali na pia inaendelea kuwa na ufaulu mzuri wa wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne kila mwaka.


“Tangu shule hii ianzishwe ufaulu wa kidato cha nne umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka. Elimu hii ya kidato cha nne inawajengewa wanafunzi msingi mzuri wa kujiunga na elimu ya juu. Pia imetujengea uwezo mzuri wa kujitambua na kufikiri,” risala hiyo iliongeza.


Wanafunzi katika risala yao pia walisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya huduma ya maji na kuomba Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuitupia macho kwa hatua za utatuzi, ili kulinda usalama wa afya za wanafunzi, walimu na wafanyakazi wa shule hiyo.


Jumla ya wanafunzi 111 (wavulana 58 na wasichana 53) wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Taifa wa kuhitimu kidato cha nne Novemba mwaka huu.


Wakati huo huo, wanafunzi hao kupitia igizo lao maalumu waliwataka vijana kujiepusha na vitendo vya uhalifu, ukiwemo uvamizi katika mgodi wa Barrick North Mara kwani vinaweza kukatisha ndoto zao kielimu,kuhatarisha maisha yao sambamba na kufifisha jitihada za uwekezaji nchini.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages