Breaking

Monday 23 October 2023

USHIRIKISHWAJI WANANCHI UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJITAKA



Diwani wa Kata ya Kawe, Wilaya ya Kinondoni Mhe. Mutta Lwakatare ameishauri Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuongeza wigo wa utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa mradi mkubwa wa uondoshaji majitaka Mbezi beach ili kila mmoja aweze kushiriki na kusaidia katika kuboresha usafi wa mazingira kwenye maeneo hayo.

Ametoa kauli wakati wa mkutano na wananchi na uongozi wa Kata kwa lengo la kujadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye kata hiyo.

Amesema kuwa mradi huu wa uondoshaji majitaka Mbezi beach ni muhimu sana na mwananchi wameupokea kwa furaha mradi huo unaolenga kuondoa changamoto inayosumbua eneo hili hasa kipindi cha mvua ambapo wakazi wasio waaminifu hutiririsha majitaka kwenye barabara za mitaa na kusababisha hatari ya magonjwa ya mlipuko.

Amebainisha kuwa Serikali kupitia DAWASA imewekeza fedha nyingi katika kutekeleza mradi huu na mategemeo ya wananchi ni kuona kero hii iliyodumu kwa muda mrefu inafika ukomo, hivyo kuwataka DAWASA kuongeza bidii ya kuwaelimisha wananchi wajue nia njema ya Serikali, manufaa ya mradi ili waweze kushiriki vyema katika kulinda miundombinu itakayowekwa kwenye mradi huu.

"Niwapongeze DAWASA kwa kazi nzuri mnayofanya ya kutekeleza mradi huu na nimeona kazi inaendelea kwenye mitaa mbalimbali, hivyo niwakumbushe kulisimamia hili ili tija ya kazi hii ionekane kwa wanufaika." amesisitiza Mhe. Lwakatare.

"Nina uhakika elimu ikitolewa kwa wingi wananchi wakaelewa wataacha tabia ya kutupa taka ngumu kwenye miundombinu ya uondoshaji majitaka na kuweza kuokoa uharibifu wa miundombinu hii," amesema.

Mbali na hapo amewataka viongozi wote wa mashina kushirikiana vyema na Mamlaka kwa kuwaonesha maeneo na mitaa yote yenye changamoto ili wajue namna ya kupitisha bomba na kurahisisha utekelezaji wa kazi.

Ametoa onyo kwa mwananchi yeyote kuacha kufungulia majitaka mitaani kwani kwa kufanya hivyo kunahatarisha afya za wananchi wengine, pia inaleta uchafuzi wa Mazingira hususani kwenye maeneo ambayo watoto huwa wanacheza.

Kwa upande wake Mhandisi wa mradi kutoka DAWASA, John Romanus amesema kuwa Mamlaka imeanza utekelezaji wa mradi huu na kazi inaendelea vizuri, ushirikiano wa wananchi na uongozi wa Kata ni wa muhimu sana kwa kuwa utaleta tija na kuwezesha malengo ya mradi kuweza kufikiwa kikamilifu.

Ameongeza kuwa Mamlaka itaendelea kuongeza elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa mradi huu pamoja na namna mradi unavyotekelezwa kwenye maeneo yao ili kila mmoja waweze kutoa mchango wake katika hili.

"Tayari mkutano mkubwa wa kuutambulisha mradi kwa ngazi ya kata umefanyika ukihusisha ofisi ya Mkuu wa Wilaya na ofisi ya Mbunge na tutaendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu mradi huu." amesema Mhandisi Romanus.

Ameeleza hadi sasa utekelezaji umefikia zaidi ya asilimia 15 na kazi ya ulazaji wa mabomba inaendelea kwenye maeneo yaliyoainishwa kwenye usanifu wa mradi.

Mradi wa uondoshaji majitaka wa Mbezi beach, ni mradi unaotekelezwa na DAWASA kwa lengo la kuboresha Usafi wa Mazingira kwenye Kata nne za ambazo ni Kata ya Mbezi Beach, Kunduchi, Salasala na Kawe ambapo wananchi takribani 11,480 watanufaika. Mradi umegharimu bilioni 124 na utakamilika ndani ya miezi 18.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages