Breaking

Thursday, 26 October 2023

TUME YA MIPANGO YARIDHISHWA UTEKELEZAJI MRADI WA KIMKAKATI BWAWA LA KIDUNDA

Ofisi ya Rais-Tume ya Mipango imetembelea Mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro kwa lengo la kuona utekelezaji na kupokea taarifa ambapo imewapongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kwa usimamizi mzuri wa Mradi tangu kuanza kwake Julai mwaka huu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Afisa Uchumi Mwandamizi Ndugu Khalid Shekimweri ameeleza kuridhishwa na hali ya utekelezaji wa mradi pia ametoa rai kwa DAWASA kuendelea na kasi katika utekelezaji ili kufanikisha mradi kukamilika kwa wakati na pia kufanyia kazi kwa wakati changamoto zilizopo ili kuondoka vikwazo vinavyoweza kuchelewesha utekelezaji.

"Tunawapongeza kwa kazi nzuri inayoendelea hapa, kazi inaonekana tunaamini ni kwasababu ya usimamizi mzuri hivyo tunawapongeza kwenye hilo, penye changamoto zitatuliwe kwa wakati ili kuondoa vikwazo kwenye utekelezaji" amesema Ndugu Shekimweri

Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi wa Kidunda Mhandisi Christian Christopher ameieleza Tume ya Mipango kazi zilizofanyika hadi sasa ikiwemo ujenzi wa barabara yenye umbali wa takribani kilomita 70 ili kurahisha mawasiliano, uchimbaji kwenye eneo la ujenzi wa mradi, ujenzi wa jengo maalum la kuhifadhi miamba na udongo baada ya upembuzi yakinifu uliofanyika katika eneo la ujenzi wa bwawa pamoja na ujenzi wa kambi ya Mkandarasi na makazi ya kudumu ya wataalamu watakaohusika kipindi chote cha ujenzi.

"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha zaidi ya bilioni 300 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi ambapo hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa malipo ya awali ( advance payment) kiasi cha bilioni 49, hadi sasa tumefikia asilimia 15 na kazi bado inaendelea tumepokea maelekezo na tunaahidi kuendelea kusimamia kikamilifu ili kutekeleza kwa wakati" amesema Mhandisi Christopher

Tume ya Mipango iliyopo chini ya Ofisi ya Rais imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Mipango ya 2023 ambapo majukumu yake ni pamoja na kupanga, kuratibu na kusimamia mipango ya maendeleo ili kuwa na mfumo jumuishi wa ufatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa vipaombele vya maendeleo ya Taifa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages