Breaking

Thursday, 12 October 2023

TEA YAJIVUNIA WANUFAIKA 49,000 WA MFUKO WA KUENDELEZA UJUZI

Mamlaka ya Elimu nchini TEA imesema inajivunia kuwa na wanufaika zaidi ya 49,000 nchi nzima walionufaika na mafunzo ya kuongeza ujuzi yaliyoendeshwa na vyuo mbalimbali chini ya mfuko wa kukuza ujuzi unaoratibiwa na mamlaka hiyo.

Akizungumza wakati wa kilele cha Juma la Elimu ya Watu Wazima ambalo maonesho yake kitaifa yanafanyika wilayani Kibaha mkoani Pwani, afisa habari wa Mradi wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) Bi. Eliafile Solla amesema kuwa wengi wa wanufaika hao kwa sasa wamejiajiri na waliosalia wameajiriwa kutokana na mafunzo waliyoyapata.

“Kwa wale waliojiajiri wameendelea kukuza wigo wa ajira kwa kuendelea kuajiri watu wengine kwenye shughuli zao za kibiashara”

Mafunzo ya kuongeza ujuzi yanayotolewa na vyuo mbalimbali vyenye ithibati kutoka wizara ya elimu, sayansi na teknolojia yamejikita kwenye maeneo sita ya kipaumbele ya kilimo na kilimo uchumi, uchukuzi, ujenzi, teknolojia ya habari na mawasiliano, utalii na huduma za ukarimu.

Maadhimisho ya “Juma la Elimu ya Watu Wazima” linatarajiwa kufikia tamati Ijumaa, Oktoba 13 mwaka huu huku idadi ya watu wazima wanaojua kusoma na kuandika ikitajwa kuongezeka.


Wadau mbalimbali wa masuala ya Elimu wakipata Elimu kwenye banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika maonesho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yanayoendelea Wilayani Kibaha, mkoani Pwani. Maonesho hayo yameanza Octoba 9 na yatafungwa rasmi Octoba 13, 2023
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages