Breaking

Tuesday, 3 October 2023

TCRA YAAHIDI KUENDELEA KUUNGA MKONO WANAHABARI WA MITANDAO YA KIJAMII

 


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanahabari ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Bw. Shabani Matwebe, akiweka wazi shughuli zinazofanywa na Jukwaa hilo mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari, aliyetembelea Ofisi za Jukwaa hilo zilizopo Sinza jijini Dar es Salaam, siku ya Jumanne, Oktoba 2, 2023, ili kujionea utendaji kazi wa Jukwaa hilo. PICHA: TCRA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari, akitoa maelezo na kujibu maswali kutoka kwa wanachama wa Jumuiya ya Wanahabari ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) wakati wa ziara yake kwenye Ofisi yao iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam siku ya Jumanne, Oktoba 3, 2023. TCRA ilitembelea Ofisi za JUMIKITA ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja. PICHA: TCRA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari (katikati), akizungumza na Meneja wa Masuala ya Wateja na Watumiaji wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano-TCRA, Bw. Thadayo Ringo, muda mfupi baada ya kuhitimisha ziara yake kwenye Ofisi za Jumuiya ya Wanahabari ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) iliyofanyika Jumanne, Oktoba 3, 2023, Sinza, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya TCRA kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2023. 
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanahabari ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Bw. Shabani Matwebe, akitoa ufafanuzi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari, kuhusu shughuli za uzalishaji wa maudhui kwa ajili ya mitandao inayofanywa na wanachama wa Jukwaa hilo katika chumba cha kuandaa maudhui hayo (Studio) kilichopo kwenye Ofisi za jukwaa hilo, Sinza jijini Dar es salaam. Mkurugenzi Mkuu Dkt Jabiri alitembelea Ofisi za JUMIKITA Jumanne Oktoba 3, 2023. PICHA: TCRA

Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt Jabiri Bakari, ameahidi kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) itaendelea kuunga mkono wanahabari wa mitandao ya kijamii nchini na kuratibu utatuzi wa baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo huku akisisitiza waandaaji na wapakiaji wa Maudhui mtandaoni kuzingatia kanuni, sheria na miongozo ya Maudhui bora ili kukidhi matakwa ya walaji.


Akizungumza katika ziara yake kwenye ofisi za Jukwaa la Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) zilizopo Sinza jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara yake ikiwa ni sehemu ya TCRA kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Dkt Bakari alisema TCRA itaendelea kuunga mkono juhudi za wanahabari hao katika kutoa taarifa sahihi na za uhakika kwa jamii na kuhakikisha kazi wanayofanya inawaletea tija zaidi.


"Tunataka jamii ipate taarifa ambazo ni nzuri na zinazokidhi ubora wa habari," alisisitiza Dkt Bakari.

Akizungumzia maudhui kwenye mitandao kuwanufaisha waandaji, Dkt Bakari alisisitiza umuhimu wa vijana kuandaa maudhui yenye tija yatakayowezesha waandaji kupata manufaa, yakiwemo manufaa ya kifedha na kwamba TCRA itaendelea kushughulikia baadhi ya changamoto zinazowakabili JUMIKITA ikiwa ni pamoja na changamoto za usajili zinazohusu taasisi nyingine.

"Tunafanya kazi na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuona kwamba tunakuwa na maudhui mengi kwa lugha ya Kiswahili," alisema Dkt Bakari.


Awali, mmoja wa wanachama wa JUMIKITA aliuliza swali akitaka kujua nini TCRA inafanya ili kuwawezesha watengeneza maudhui kunufaika kwa maudhui wanayopakia kwenye mitandao.

Akijibu swali hilo, Dkt Bakari alisema TCRA wanalichukua suala hilo na wataendelea kulifanyia kazi.

"Tuna role kubwa sana ya kuiandaa hii jamii kupata maudhui yanayojenga, na yanayoweza kuifaidisha jamii," alisema Dkt Bakari.


Ziara ya Dkt Bakari katika ofisi za JUMIKITA ni sehemu ya juhudi za TCRA za kuendelea kuunga mkono vyombo vya habari nchini na waandaaji wa Maudhui yenye kuinufaisha Tanzania na wananchi. TCRA ni taasisi ya Serikali iliyoasisiwa mwaka 2003 mwezi Novemba ili kusimamia sekta ya mawasiliano ya kielektroniki na Posta. Sekta zinazosimamiwa na Mamlaka hiyo ni pamoja na Simu, Intaneti, Utangazaji na Posta.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages