Breaking

Monday, 16 October 2023

TBS YAWATAKA WADAU KUSHIRIKI KATIKA MASHINDANO YA TUZO ZA UBORA ZA KITAIFA 2023

Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania, TBS, Shirika la Viwango Zanzibar, ZBS pamoja na Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), imeandaa tuzo za ubora za kitaifa awamu ya nne kwa 2023 kwa wajasiriamali, wazalishaji wa viwandani na watoa huduma,lengo ni kutambua na kuthamini wadau ambao wameonesha mchango mkubwa katika maendeleo ya ubora.

Madhumuni ya tuzo hizo ni kuendelea kujenga utamaduni wa ubora (quality culture) na ushindani katika shughuli za huduma na uzalishaji hapa nchini, kuhamasisha wadau kuzingatia na kutumia mbinu za ubora katika shughuli za uzalishaji bidhaa na huduma, kukuza uelewa wa pomoja wa kanuni za ubora, mbinu za kibiashara na viwango kukuza ushindani, Kutangaza na kuweka imani kwa watumiaji wa bidhaa aidha ndani ya nchi au nje ya nchi kuwa bidhaa zinazo zalishwa nchini zinafata misingi na kanuni za ubora.

Akizungumza na waandishi wa habari Oct 13,2023, Afisa ubora mwandamizi wa TBS, Bw.Athumani Kissumo amesema Shirika linawasisitiza watoa huduma, wazalishaji wa bidhaa na wajasiriamali kushiriki katika tuzo hizo kwani zitawafanya watambulike kitaifa, kikanda na kimataifa.

Pamoja na hayo alieleza kuwa kutakuwa na vipengele vitano vya tuzo ambavyo ni Kampuni Bora ya mwaka,bidhaa Bora ya mwaka,mtoa huduma Bora wa mwaka,Msafirishaji Bora wa bidhaa nje nchi wa mwaka, na kipengele cha mwisho ni cha mtu ambaye amefanya vizuri katika masuala ya ubora. Alieleza kuwa kila kipengele kitagusa mzalishaji mkubwa na mjasiriamali isipokuwa kipengele cha mtu aliefanya vizuri katika maswala ya ubora ambapo kutakuwa na mtu aliefanya vizuri katika maswala ya mifumo ya ubora na aliefanya vizuri katika maswala ya kiufundi ya ubora ikiwemo kwenye uzalishaji.

Kwa Upande wake Mkuu wa kitengo cha biashara wa TPSF Bw. Gaspa Kahungya ametoa wito kwa wafanyabiashara kujitokeza ili waweze kushiriki katika tuzo hizo ambazo zitawaongezea wigo wa biashara zao.

"Tunatamani wafanya biashara na wazalishaji wajitokeze kwa wingi kwani watanzania wanazalisha bidhaa Bora ila kutokana na kutokuwepo kwa mashindano haya bidhaa zimekuwa hazitoki, hivyo basi mashindano haya yanaanzia nchini na yataenda Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC na Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Africa, SADC" Amesema

Fomu ya maombi kushiriki tuzo hizo inapatikana kwenye tovuti, Shirika la Viwango, TBS, www.tbs.go.tz, au Shirika la Viwango la Zanzibar, ZBS www.zbs.go.tz, tivuti ya TPSF, www.tpsf.org. Tarehe ya mwisho ya kupokea maombi kwa washiriki ni mwezi Oktoba 20,2023 saa 5:59 usiku,maombi yaelekezwe kwenda National Qulity Award Secretariat, Tanzania Bureau Of Standards, P. 0 Box 9524, Dar es Salaam au tuma barua pepe qualityawards@tbs.go.tz au info@zbs.go.tz. Kampuni itakayo shiriki iwe imesajiliwa nchini, taarifa ziwe sahihi kwa ufupi, tuzo hizo zitarajiwa kufikia kilele Nov 10,2023 ambayo ni siku ya ubora kitaifa.
Afisa ubora mwandamizi wa TBS, Bw.Athumani Kissumo akizungumza na waandishi wa habari Oct 13,2023 Jijini Dar es Salaam wakati wakitoa taarifa kuhusu uandaaji wa tuzo za ubora za kitaifa awamu ya nne kwa 2023 kwa wajasiriamali, wazalishaji wa viwandani na watoa huduma

Mkuu wa kitengo cha biashara wa TPSF Bw. Gaspa Kahungya akizungumza na waandishi wa habari Oct 13,2023 Jijini Dar es Salaam wakati wakitoa taarifa kuhusu uandaaji wa tuzo za ubora za kitaifa awamu ya nne kwa 2023 kwa wajasiriamali, wazalishaji wa viwandani na watoa huduma

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages