Na Mwandishi Wetu, Njombe
WAJASIRIAMALI wanaozalisha bidhaa za aina mbalimbali wameshauriwa kuthibitisha ubora wa bidhaa ili kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.
Hatua hiyo itawawezesha kuongeza ubora wa bidhaa zao, kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi na kuzalisha bidhaa ambazo zina uwezo wa kushindana katika soko la Tanzania, Afrika Mashariki na Dunia kwa ujumla.
Ushauri huo umetolewa leo na afisa Uhusiano wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Neema Mtemvu, wakati wa akizungumza na wajasiriamali kwenye Maonesho ya Nne Kitaifa ya SIDO yaliyoanza Oktoba 21, mwaka huu na yatamalizika kesho (Oktoba 31) mkoani Njombe.
Mtemvu alisema wameshiriki maonesho hayo ili kueleza huduma ambazo zinatolewa na TBS, kwani wao ndiyo wanaohusika na kusajili na kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa nchini na zile zinazotoka nje zinakidhi vigezo vyote vya ubora.
Kwa mujibu wa Mtemvu Serikali ina mpango wa kukuza viwanda vidogo na vya kati wa wajasiriamali, hivyo TBS kwa kushirikiana na SIDO wana programu ya kuhakikisha wajasiriamali wanazalisha bidhaa ambazo zina ubora na zinazoweza kushindana sokoni.
Alisema wajasiriamali wanatakiwa kupitia SIDO na kupatiwa mafunzo mbalimbali yanayohusiana na bidhaa wanazozalisha, kisha wataandikiwa barua ya utambulisho kwenda TBS.
"TBS tukishapata barua ya mjasiriamali, tutampatia huduma na leseni ya kutumia alama ya ubora ya TBS bure bila gharama yoyote. Atatumia miaka mitatu bila kulipia gharama yoyote na kuanzia mwaka wa nne kadri itakavyoonekana ataanza kulipa asilimia 25 ya ile ada ambayo alitakiwa ailipe," alisema na kuongeza.
"Huduma hii inawasaidia wajasiriamali wote kuhakikisha kwamba bidhaa zao zinakidhi vigezo vya ubora.
Kwa sababu hiyo, Mtemvu alisema wana jukumu kubwa la kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa na wajasiriamali nazo zinakidhi ubora.
Alifafanua kuwa wanataka bidhaa hizo ziwe na uwezo wa kutumika hapa nchini na hata nje ya nchi, kwa sababu zikishathibitishwa zitakuwa na ubora unaokubalika.
Wajasiriamali waliotembelea banda la TBS kwenye maonesho hayo ili kufahamu ni kwa namna gani bidhaa zao zinaweza kuthibitishwa ili kuwezesha wateja wengi na kupata kilicho bora na kinachoaminiwa na Serikali, walipongeza utaratibu huo na kwamba baada ya maonesho hayo wanaenda kuanza safari ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao.
Walisema maofisa wa TBS wamewaelekeza namna ya kufanya, hivyo alishukuru uongozi wa shirika hilo na shirika hilo, SIDO na Serikali kwa kuwa na mpango wa kuwainua wajasiriamali.
Afisa Udhibiti Ubora (TBS), Bi.Doris Mchwampaka akitoa elimu kuhusu masuala ya Viwango kwa wananchi waliotembelea banda la TBS katika maonesho ya nne ya SIDO yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba mkoani Njombe