Breaking

Wednesday, 4 October 2023

PRO.MKUMBO AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUFUNGAMANISHA SERA NA MIPANGO YA TAASISI NA MIPANGO YA TAIFA

Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ametoa rai kwa Taasisi za Umma kuhakikisha zinafungamanisha Sera na Mipango ya taasisi hizo na Mipango ya Taifa ili kuwa na matumizi yenye tija kwa Rasilimali za nchi.

Prof. Mkumbo ameyasema hayo Octoba 4, 2023 mkoani Dodoma katika kikao kilichowakutanisha na Waziri wa Madini Mhe. Antony Mavunde kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa utekelezaji wa majukumu kati ya Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Wizara ya Madini.

Katika kikao hicho Mawaziri hao wamejifunza na kubaini Mipango ya Maenendeo na fursa za uwekezaji katika sekta ya madini ili kuzitangaza duniani.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema Wizara yake imepanga hadi kufika mwaka 2030 iwe imefanya utafiti wa kina wa kijiologia na jiofizikia kwa ajili ya kupata taarifa ya miamba na madini kufikia asilimia 50 ambapo kwa sasa ni asilimia 16 tu iliyofanyiwa utafiti wa maeneo yenye madini nchini.

Waziri Mavunde ameongeza kuwa uchumi wa madini unaonekana kwa sasa unatokana na asilimia 16 ya eneo lililofanyiwa utafiti wa kina akitolea mfano katika mwaka wa fedha 2022/2023 sekta ya madini imeongoza kwa mauzo ya bidhaa za nje kwa asilimia 56 ambapo mauzo yamefanyika kwa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 3.3.

Aidha, sekta hiyo ya madini imechangia katika kodi ya mapato ya ndani kwa asilimia 15 ambayo ni zaidi ya trilioni 2 za kitanzania.

Vilevile, Mavunde ameongeza kuwa taarifa zitakazopatikana kupitia tafiti hizo hususan tafiti za miamba zitasaidia Wizara ya maji kufahamu maeneo yanayofaa kuchimba visima vya maji na pia tafiti hizo zitasaidia Wizara ya kilimo kwa ajili ya uchimbaji wa mabwawa na kilimo cha umwagiliaji ili watanzania waepukane na kilimo cha kutegemea mvua.

Waziri Mavunde, alisisitiza tafiti zinazoendelea kufanyika zitasaidia wachimbaji wadogo kufahamu maeneo yenye madini na kuondokana na adha ya kupata hasara kutokana na hali ya sasa ilivyo ya wachimbaji wengi kukisia maeneo ya uchimbaji. Pia, tafiti hizi zitaondoa migogoro kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo kwa kuwa uchimbaji utafanyika kwa katika maeneo yaliyofanyiwa tafiti.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages