Breaking

Wednesday, 4 October 2023

PROF. OREKU: TAFITI BORA, CHANZO CHA MAPATO

Tafiti na machapisho yenye kukidhi ubora wa ushindani yanaweza kukisaidia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) katika kupata ufadhili na miradi itakayosaidia kuongeza mapato ya ndani ya chuo.

Hayo yamesemwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anayesimamia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. George Oreku, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya uandishi wa mapendekezo ya utafiti yenye viwango vya juu vya ubora na shindani, Oktoba 03, 2023 katika shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha, mkoani Pwani.

“Kurugenzi yetu ya Utafiti, Machapisho na Ubunifu imeundwa kwa lengo kuitumikia taasisi yetu kuhakikisha tafiti, machapisho na bunifu zinazotoka zinakuwa na ubora unaokidhi viwango vya hali ya juu. Hapa tunawajengea uwezo wahadhiri kuweza kuandika mapendekezo ya utafiti yenye viwango vya kiushindani ili maandiko yao yaweze kushinda na hili ni muhimu sana kwa kuongeza mapato ya chuo na kusaidia shughuli nyingine za kimaendeleo za chuo.” Amesema Prof. Oreku.

Aidha, aliendelea kueleza kuwa mapendekezo ya utafiti yakiandikwa vizuri Kitaalamu na kibobezi yatashinda na kuwa pia ni sehemu ya kukitangaza chuo na kukaribisha wafadhili na wadau wa maendeleo ambao watawekeza kwa kuanzisha miradi mbalimbali kwa kushirikiana na chuo.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti, Machapisho na Ubunifu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Harrieth Mtae, amesema mafunzo haya yanalega kuongeza ujuzi wa uandishi wa kiushindani kwa wanataaluma wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika kuandika mapendekezo ya utafiti na miradi itakayoshinda kutokana na ubora wake.

“Mafunzo haya ni ya awali, tunataraji kuyafanya mafunzo mengi zaidi kama haya ili washiriki wawe na uwezo wa kuandika maandiko hasa mapendekezo ya utafiti yenye ubora wa viwango vya juu na kushinda ili kupata fedha za kuanzisha na miradi mbalimbali. Pia, mafunzo haya ni utekelezaji wa mpango mkakati wa chuo pamoja na ajenda ya utafiti ya chuo, ambazo zote zinachagiza uwepo wa machapisho na tafiti nyingi zenye kutatua matatizo ya jamii nchini." Amesema Dkt. Mtae.

Akizungumza katika Mafunzo hayo, Mratibu Mwandamizi wa Tafiti kutoka COSTECH, Bi. Bestina Daniel, amewakumbusha watafiti kusajili tafiti zao na kupata kibali kabla ya kuanza kufanya utafiti ili kuhakikisha zinafuata sheria, maadili na taratibu za nchi.

“Wakati mwingine tafiti hasa za kimataifa zinazohusisha watafti kutoka nje ya nchi zinaweza kuwa ni tafiti ambazo kwao ni sahihi lakini nchini kwetu zikawa haziendani na sheria, tamaduni au miiko yetu, hivyo usajili wa tafiti ili kupata kibali ni muhimu sana kwa watafiti wote.” Amesema Bi. Bestina.

Mafunzo haya ya siku tano ya uandishi wa mapendekezo ya utafiti yenye ubora yanayoendelea katika shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha, mkoani Pwani. Mafunzo haya yanasimamiwa na kurugenzi ya Utafiti, Mchapisho na Ubunifu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. yameanza Oktoba 2 na yanatarajiwa kumalizika Oktoba 6, 2023. Watumishi mbalimbali wa chuo hiki wanashiriki katika mafunzo hayo ambayo yanalenga kuongeza wingi wa tafiti lakini pia ubora wa tafiti na machapisho chuoni. Dkt. Edefonce Nfuka amepata heshima ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa majadiliano katika mafunzo hayo kwa siku zote tano za mafunzo hayo. Dkt. Nfuka ni Mkurugenzi wa huduma za ushauri wa kitaalamu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages