Na: Zainab Ally - Nyerere
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Benedict Wakulyamba amesema miradi inayotekelezwa na Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) utachochea ongezeko la watalii wanaoitembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere punde utakavyokamilika.
Kamishna Wakulyamba amebainisha hayo mwishoni mwa wiki hii, alipotembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere na kukagua miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia REGROW ambapo jumla ya Miradi 22 itakayogharimu zaidi ya shilingi bilioni 141 ikitekelezwa Kusini mwa Tanzania.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo aliendelea kutoa dira ya Wizara katika mkakati wa kukuza utalii ambapo alisema miradi hiyo itaongeza uwezo wa ufanyaji kazi kwa watumishi ambapo vituo mbalimbali vya kutoa taarifa kwa wageni vikitarajiwa kuongezwa.
“Ndugu zangu huu mradi wa Benki ya Dunia wa kuboresha Maliasili zetu unafanya mambo makubwa sana. Kuna changamoto nyingi za uharibifu wa Mazingira yanayosababishwa na shughuli za wananchi na mabadiliko ya tabia ya nchi, sasa mradi huu wa REGROW unaanza kurejesha uhai wa mito yetu katika usimamizi bora wa maji”, alisema Kamishna Wakulyamba.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Herman Batiho aliwataka wasimamizi wa miradi inayoendelea kutekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Nyerere kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati kwa kufuata viwango vya ubora wa Kimataifa.
“Serikali imejipambanua kupitia Filamu ya (The Royal Tour) juu ya vivutio vyetu, wageni wengi wanakuja na wanataka kuutumia uwanja huu wa ndege, tujitahidi tusiwe kikwazo kwa kukamilisha Uwanja huu ili tuongeze idadi ya Watalii kama ilivyo katika Ilani ya CCM kufikia wageni Milioni tano”, alisema Batiho.
Nae, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ephraim Mwangomo, alisema hifadhi hiyo imejipanga kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuendelea kutoa huduma bora kwa watalii na usalama wao pamoja na kushiriki katika kuendeleza jamii zinazozunguka Hifadhi ya Taifa Nyerere.
Aidha, Mwangomo alitoa taarifa ya ongezeko la makundi ya wageni wa nje ambapo mpaka kufikia mwaka 2022 jumla ya shilingi bilioni 10.9 zilikusanywa, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuongeza kipato ikiwa wawekezaji watajitokeza katika uwekezaji miundombinu ya nyumba za wageni.
“Tunatazamia maboresho ya miundombinu hii inayoendelea ya Viwanja vya ndege, tukija kupata wawekezaji wakijenga nyumba za wageni, tuna matarajio ya kuongeza makusanyo kutokana na upekee wa hifadhi hii,” alisema Mwangomo.
Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) unatajwa kufungua milango ya utalii katika hifadhi zilizopo Kusini mwa Tanzania ambapo itachagiza ongezeko la makundi ya watalii kwa uwepo wa miundombinu rafiki ndani ya hifadhi za taifa zilizojumuishwa katika mradi huo.