Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Jasmin Kairuki (Mb) anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye mkutano wa 24 wa Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori ya Afrika utakaofanyika kuanzia jijini Arusha kesho Oktoba 30 hadi Novemba 3, 2023.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyosainiwa na Mhe. Kairuki, Mkutano huo utafanyika sambamba na Wiki ya Misitu na Wanyamapori ya Afrika ya Nane (AFWW8) katika Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha, Tanzania.
Serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Ishirini na Nne (24) wa Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWC24)
Taarifa hiyo imefafanua kuwa Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori ya Afrika (AFWC) ni moja ya Kamisheni sita za Misitu za Kikanda za FAO, ikiwa ni mamlaka ya kisheria ya juu ya Afrika katika masuala ya misitu na wanyamapori. Ni jukwaa maalum ambapo viongozi wa misitu na wanyamapori kutoka nchi wanachama wa Afrika wanakutana kila miaka miwili kujadili masuala muhimu, kukuza umoja wa kikanda na kuchangia katika ajenda ya ulinzi wa mazingira ya dunia.
Imeongeza kuwa, ikiwa na wanachama 53, AFWC24 inatarajiwa kuwavuta washiriki wa aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wawakilishi kutoka nchi wanachama, Umoja wa Mataifa (UN) na mashirika ya kimataifa, mashirika ya kiraia, makundi ya vijana, wadau wa maendeleo, na Sekta Binafsi.
Mkutano huu unatarajiwa kuwaleta pamoja washiriki takriban 350 kutoka nchi wanachama na tasisi shiriki, na utahusisha matukio mbalimbali ambayo yatawapa nafasi wadau mbalimbali kuonyesha juhudi zao za uhifadhi wa wanyamapori na misitu na kukuza ushirikiano.
Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori ya Afrika (AFWC) ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa ilianzishwa mwaka 1959 na inatekeleza jukumu muhimu la kuwawezesha nchi wanachama kujadili na kutatua masuala muhimu ya misitu na wanyamapori katika ngazi ya kikanda katika mikutano inayofanyika kila baada ya miaka miwili.
Aidha taarifa hiyo imefafanua kuwa Tanzania kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inayo furaha kuwakaribisha wajumbe wote ambao wataungana nasi kwa AFWC24 na AFWW8.
Kwa upande wa Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amesema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika.
Amefafanua kuwa Mkutano huu una mchango mkubwa katika kutengeneza mustakabali wa sekta za misitu na wanyamapori Tanzania na barani Afrika, na kuhakikisha usimamizi endelevu kwa manufaa ya bara la Afrika na dunia kwa ujumla.