Breaking

Wednesday, 4 October 2023

MADARAJA YA MAWE YANEEMESHA WANANCHI KIGOMA

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Octavian Mshiu, amewaambia waandishi wa habari mkoani Kigoma kuwa mkoa huo umekuwa kinara katika ujenzi wa madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe na kwamba madaraja hayo yameonyesha ufanisi wa hali ya juu katika ubora na urahisi wa kufungua barabara vijijini kutokana na gharama za ujenzi wake kuwa nafuu zaidi.

Mshiu amesema kuwa Bodi hiyo imeamua kutembelea madaraja hayo yanayojengwa kwa teknolojia mbadala ya kutumia mawe ili kuona namna ya kusaidia kuisambaza teknolojia hiyo iweze kutumika kwa wingi zaidi nchini na hivyo kuipunguzia Serikali gharama za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya madaraja lakini pia kusaidia kufungua barabara za vijijini kwa kasi zaidi.

“Mkoa wa Kigoma kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), umejenga jumla ya madaraja 110 kwa gharama ya shilingi bilioni2.4 kiasi ambacho ni nafuu zaidi kwani madaraja hayo yangejengwa kwa nondo na saruji kama tulivyozoea ujenzi wake ungegharimu zaidi ya shilingi bilioni 11, hivyo madaraja haya 110 yameokoa zaidi ya asilimia 80 ya gharama ambazo zingetumika kwa madaraja ya kawaida. Madaraja haya pia yametoa ajira kwa wakazi wa mkoa wa kigoma ambapo zaidi ya ajira 500 zilitolewa kwa wazawa ili kutekeleza ujenzi huo, hii ni kwa sababu ujenzi wa madaraja ya mawe unatoa ajira kwa mtu yeyote bila kujali kiwango cha elimu alichonacho”, amesema Mshiu.

Akitolea mfano daraja la Nyamihanga lililoko wilaya ya Buhigweambako mahojiano haya yamefanyika, Mshiu amesema kuwa daraja hilo ambalo liko kwenye hatua za mwisho za ujenzi wake lina urefu wa mita 32 na upana wa mita 6 na kwamba limegharimu kiasi cha shilingi milioni 159 ambapo kati ya hizo shilingi milioni 70.3 ni fedha za Mfuko wa Barabara.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Mfuko wa Barabara amefafanua kuwa katika hali ya kawaida daraja hilo la Nyamihanga iwapo lingejengwa kwa mfumo wa zege lingegharimu kiasi cha shilingi milioni 780 fedha ambayo ingeweza kugawanywa katika miradi mingine ya huduma za kijamii kama vile afya na elimu.

“Eneo tulilopo linaitwa Kwitanga, tunaambiwa magari hayajawahi kuvuka upande wa pili wa mto Luiche kwenda Muzeze tangu tupate uhuru au tangu dunia hii imeumbwa, lakini kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita barabara hii itafunguliwa hivi karibuni na magari yataweza kuvuka kutoka upande wa Kwitanga kwenda Muzeze” ameongeza Mshiu.

Akiongea kwa niaba ya wakazi wa Kwitanga Zuwena Kwilelula ameiomba Serikali kukamilisha kwa haraka ujenzi wa daraja hilo la Nyamihanga ili waweze kunufaika na huduma za kijamii upande wa Muzeze ambako kuna zahanati na mashamba ya maharage lakini pia waweze kusafirisha mazao yao kutoka Muzeze kwenda Kwitanga na baadae kuyapeleka sokoni kwa urahisi.

Awali akiwasilisha taarifa yake mbele ya wajumbe wa bodi, Mhandisi Felician Kavishe kutoka TARURA mkoa wa Kigoma alisema kuwa TARURA mkoa wa Kigoma imejenga jumla ya madaraja 110 katika mkoa huo ambapo madaraja 35 yako Wilaya ya Kigoma, 20 wilaya ya Kasulu, 6 wilaya ya Buhigwe, 15 Uvinza, 19 Kibondo na 15 Kakonko

Ameongeza kuwa TARURA Kigoma imetumia kiasi cha shilingi milioni 383.32 kutoka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya ununuzi wa mawe yaliyotumika katika ujenzi wa madaraja 13 ya mawe mkoani humo.

Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wako mkoani Kigoma kujionea jinsi teknolojia mbadala kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja inavyoweza kuipunguzia Serikali gharama za ujenzi na matengenezo ya barabara nchini.Muonekano wa Daraja la Mawe la Bweru mkoani Kigoma ambalo kitaalamu limejengwa kwa mtindo wa segmental, linaurefu wa mita 26, upana mita 6.5 na limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 101, lina uwezo wa kupitisha magari yenye uzito hadi tani 40. Daraja hilo kama lingejengwa kwa zege lingegharimu shilingi milioni 505. Mfuko wa Barabara umetoa fedha kuchangia ujenzi wa madaraja ya mawe 13 mkoani Kigoma.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Octavian Mshiu, akimuelekeza jambo Meneja wa TARURA mkoa wa Kigoma Mhandisi Godwin Mpinzile (mwenye shati jeupe), wakati wajumbe wa bodi hiyo walipotembelea Daraja la Mawe la Nyamihanga lililoko mto Luiche katika eneo la Kwitanga mkoani Kigoma. Wengine ni mjumbe wa Bodi Hussein Wandwi (wa pili kushoto) na Mhandisi Felician Kavishe wa TARURA Kigoma.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Octavian Mshiu (kushoto), akiongozana na Meneja wa TARURA mkoa wa Kigoma Mhandisi Godwin Mpinzile, wajumbe wa bodi na wanahabari kwenda kukagua ujenzi wa daraja la mawe la Nyamihaga lenye urefu wa mita 32 na upana mita 6, linalojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 159.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga (kushoto) akiwaongoza wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Naibu Katibu Mkuu Ujenzi Ludovick Nduhiye (kulia) na Hussein Wandwi Baada ya kukagua daraja la Nyabigufa mkoani Kigoma lenye urefu wa mita 31, upana mita 5.5 na lenye uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa hadi tani 40.
Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara pamoja na wafanyakazi wa TARURA mkoa wa Kigoma wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukagua Daraja la Mawe Nyabigufa (Roman Arch Bridge) mkoani humo lenye urefu wa mita 31 na upana wa mita 5.5 lililojengwa kwa gharama ya shilingi 112 milioni, lina uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa hadi tani 40

Picha na Bodi ya Mfuko wa Barabara
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages