Breaking

Tuesday, 31 October 2023

KITUO CHA MABASI CHA KISASA CHENYE THAMANI YA SH.13 BILIONI KUJENGWA GEITA

KUPITIA Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTS) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) inatarajia kujenga kituo cha mabasi cha kisasa mjini Geita chenye thamani ya shilingi bilioni 13.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 31,2023 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi mara baada ya kukagua eneo lililotengwa kwa mradi huo ambalo limemegwa kutoka hifadhi ya msitu wa Usindakwe.

Zahara amesema kituo hicho cha mabasi (stendi) kinakwenda kutatua kero ya muda mrefu kwa mji na mkoa wa Geita kwani stendi ya sasa haina ubora wa miundombinu inayostahimili kutoa huduma bora.

“Hatuna stendi yenye hadhi ya mkoa wenye dhahabu na madini, mheshimiwa Rais kwa kuliona hilo ametupatia hiyo stendi na sasa hivi tupo katika hatua ya upembuzi yakinifu na hatua za manunuzi.

“Tupo hatua za kuweza kupata mkandarasi mzuri mwenye uzoefu wa kujenga stendi hizi, zenye ubora na kuvutia katika mji wetu, kwa hiyo hizo taratibu zimeanza na zinaendelea.”

Amesema hadi Disemba, 2023 taratibu zote za awali zinatarajiwa kukamilika na mikataba itasainiwa ili utekelezaji uanze kwani halmashauri imejipanga mradi ukamilike kwa wakati na ufanisi.

“Stendi ile imelenga katika kukuza mji wa Geita, kuleta fursa mbalimbali za kiuchumi, kwani kutakuwa na sehemu ya uwekezaji wa hoteli, wafanyabiashara, wamachinga, bajaji, bodaboda, mamalishe, babalishe.

“Wakandarasi ambao wanakuja Geita na kusuasua kwenye miradi, mimi ndio mkurugenzi hapa Halmashauri ya Mji wa Geita sitowavumilia, itakuw akata mti panda mti, ukinizingua tnazinguana.”

Ofisa Mipango Miji Halmashauri ya mji wa Geita, Barbara Mustapha amesema eneo la mradi ni hekta 120 kutoka hifadhi ya msitu wa Usindakwe chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Amesema stendi pekee itatumia ukubwa wa hekta 10 huku eneo linalosalia kutakuwa na vyuo vya kati, maeneo ya biashara na pamoja maeneo ya uwekezaji.

Kaimu Mhandisi wa Miundombinu na Mratibu wa TACTIC Halmashauri ya Mji wa Geita, Mhandisi Oswald Mtei amesisitiza wapo hatua za mwisho za manunuzi na kumpata mkandarasi mradi uanze kujengwa.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages