Breaking

Friday 6 October 2023

KAMATI ZA MIRADI YA MAJI ZACHAGIZA UKAMILISHAJI MRADI WA BILIONI 65



Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imezishukuru kamati za maji za kushughulikia malalamiko zilizoundwa wakati wa utekelezaji wa mradi wa maji Makongo hadi Bagamoyo kwa kufanikisha ukamilishaji wa mradi wa zaidi ya Bilioni 65 unaohudumia wakazi takribani 450,000.

Kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kupokea taarifa za kamati hizo pamoja na kuzipongeza kamati kwa kazi nzuri waliyoifanya na kupelekea mradi kukamilika kwa wakati.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji Mhandisi Shabani Mkwanywe amezipongeza kamati hizo kwa kazi nzuri waliyoifanya na kupelekea mradi kuisha kwa wakati na kuleta matokeo chanya kwa Jamii.

"DAWASA tunawashukuru sana wajumbe wa kamati hizi katika kata zote mradi ulipopita, kazi nzuri mlioifanya imepelekea mradi kwenda kwa haraka bila kukumbana na matatizo makubwa ambayo yangeweza kukwamisha mradi huu. Matokeo ya kazi nzuri inaonekana kwa wakazi wa Makongo hadi Bagamoyo kupata na huduma bora ya Majisafi na Salama." ameeleza Mhandisi Mkwanywe.


Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo Cha Mazingira, ndugu Vivian Silayo amezitaka kamati hizo kuwa mabalozi wakudumu wa utunzaji wa miundombinu ya Majisafi na kuwatoa hofu wananchi wachache ambao huduma haijawafikia kuwa Mamlaka itakwenda kuwahudumia kuhakikisha kila mmoja anapata huduma.

"Tunatambua kwenye maeneo yenu kuna baadhi ya mitaa ambayo huduma ya majisafi haijafika, niwatoe hofu kuwa maeneo yote DAWASA itapeleka huduma na kila mmoja atapata huduma." ameeleza ndugu Silayo.


Akiongea kwa niaba ya kamati hizo, Abdallah Mbupu ameishukuru utaratibu wa DAWASA kushirikisha jamii na hasa viongozi wa Serikali za mitaa katika upangaji na utekelezaji wa miradi yao kitendo kinachoepusha mikwaruzano na malalamiko yanayoweza kukwamisha utekelezaji wa miradi.

Kamati za Kushughulikia malalamiko huundwa kwa lengo la kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kipindi cha utekelezaji wa mradi ili kufanikisha mradi kukamilika kwa wakati. Wajumbe wa kamati hizo hutokana na viongozi wa Serikali za mitaa pamoja na wawakilishi wa wananchi wanaoteuliwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages