Breaking

Saturday, 14 October 2023

KAMATI YA BUNGE YATAKA KASI ZAIDI UTEKELEZAJI MRADI WA KIDUNDA



Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda unaotekelezwa na Wizara ya Maji na kusimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) na kusisitiza ukamilishwaji wake ndani ya muda uliopangwa wa miaka 3.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Kaimu Mwenyekiti Mhe. Felix Kavijuru (Mb) imetembelea eneo la ujenzi wa mradi huo lililopo katika kijiji cha Kidunda Kata ya Mkulanzi kwa lengo kukagua maendeleo ya utekelezaji wake.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mhe. Kavijuru amesema kamati imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo wenye tija na manufaa makubwa kwa wananchi hususani wa Mikoa ya Dar es salaam na Pwani, na pia kwa wananchi wa vijiji vinne vilivyopo ndani ya Kata ya Mkulazi ambao watanufaika na fursa mbalimbali zitakazojitokeza wakati wa mradi.

"Kamati yetu imeridhika na tulichokiona eneo la mradi, mradi huu umesikika kwa muda mrefu katika vitabu lakini sasa tutaenda kuutangaza zaidi kwa wananchi, tunamshukuru Raisi wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu kwa kuruhusu fedha zaidi ya Bilioni 300 zitumike kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa hili ambalo lilikua kwenye maongezi kwa mda mrefu." amesema

Pia amesisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji kwa kuhakikisha mazingira yanatunzwa vizuri, shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi za mito na mabwawa zinadhibitiwa mapema kuepusha madhara, ameongeza kuwa kama vyanzo vya maji visipotunzwa vizuri vitaondoa maana nzima ya ujenzi wa Bwawa la kidunda kwa kuwa kutakosekana maji ya kulijaza.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) ameishukuru kamati kwa kuongeza hamasa ya uwajibikaji kwa watendaji wa Wizara ya Maji ambayo itachangia kuleta mabadiliko chanya ya kiutendaji.

" Kwanza kabisa tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Tanzania Dkt. Samia Suluhu kwa kufanya uwekezaji huu mkubwa na kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji, pili tunaishukuru sana kamati kwa kutembelea mradi na sisi kama wizara tunawaahidi kuusimamia kikamilifu." amesema Mhe. Mahundi.

Akitoa maelezo ya mradi mbele ya kamati, msimamizi wa mradi wa kidunda Mhandisi Christian Christopher amesema mradi umefikia asilimia 15 tangu uanze kutekelezwa Julai 2023, Hivvyo yunategemea kumaliza mradi ndani ya muda uliopangwa kwani mkandarasi yupo kazini na kazi inaendelea.

Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda ni mojawapo ya mradi wa kimkakati inayotekelezwa na Wizara ya maji kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Dar es salaam na Pwani, Mradi unatekelezwa kwa gharama ya bilioni 335 mbali na kuongeza upatikanaji wa maji pia mradi utazalisha umeme takribani megawati 20 ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya taifa.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages