Breaking

Sunday, 8 October 2023

WAZIRI KAIRUKI ATAJA TAREHE ZA ONESHO LA SITE 2024


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki ametangaza tarehe ya maonesho ya nane ya Swahili International Tourism Expo - S!TE, 2024 kuwa ni Oktoba 11-13 na kuwataka waandaaji kuyaboresha zaidi ili kupata washiriki wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo leo Oktoba 8,2023 katika siku ya mwisho ya Maonesho ya Saba ya Swahili International Tourism Expo- S!TE 2023 wakati akifunga maonesho hayo jijini Dar es Salaam.

Amewashukuru wadau wote walioshiriki kwenye maonesho yam waka huu ambapo amesema bila ushiriki wao lisingeweza kufanyika kwa kiwango na ubora mkubwa kama lilivyofanyika.

Ameipongeza Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kupamba maonesho haya kwa kuandaa bustani ya wanyama hai pori ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa watu waliotembelea.

Aidha amewaomba wadau kutoa maoni kuhusu maonesho ya mwaka huu ili yasaidie kuboresha maonesho ya mwakani na kuyafaya kuwa ya kimataifa.

“Maboresho haya yatatujenga na kutusaidia kutuingiza katika maonesho makubwa ya kimataifa kama vile world tourism Market.” Amefafanua Mhe. Kairuki

Awali Mhe. Kairuki alisema pamoja na kazi kubwa ya kuboresha miundombinu iliyofanywa na kusaidia kuleta watalii pia alifafanua kuwa ongezeko kubwa la watalii nchini limetokana na kazi nzuri iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya “The Royal Tour”. Filamu hii ilionyeshwa katika vituo vingi vya televisheni vinavyotambulika nchini Marekani na kwingineko duniani ili kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages