Breaking

Tuesday 17 October 2023

JENGO LA DAWASA YETU CHACHU YA KUBORESHA HUDUMA YA MAJI





Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange amesema kuwa ukamilishwaji wa jengo jipya la DAWASA yetu utachochea tija ya uimarishaji na utoaji wa huduma za Maji kwa Wananchi.

Akizungumza wakati alipotembelea jengo hili lililojengwa na Serikali kupitia Mkandarasi kampuni ya Uhandisi ya China (CCECC) amebainisha kuwa kuhamia kwa baadhi ya ofisi za DAWASA kwenye jengo hili umelenga kupisha utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa ya mwendokasi yaani SGR.

Jenerali Mwamunyange ameongeza kuwa jengo hili ni la kisasa na litachochea kwa kiasi utoaji wa huduma kwa ufanisi na kwa haraka hasahasa matumizi ya mifumo ya Tehama.

"Niwapongeze wafanyakazi wa Mamlaka kwa kutekeleza kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa zoezi la kuhamisha mali na samani kutoka kwenye ofisi za zamani zilizokuwepo eneo la Gerezani na kuja kwenye jengo jipya la DAWASA Yetu." amesema Jenerali Mwamunyange.

"Nimefurahishwa sana na kasi ya utekelezaji wa mradi wa jengo hili na tuna matumaini kuwa mradi utaleta ari kubwa ya watumishi katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi," ameeleza Jenerali Mwamunyange.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa utekelezaji wa jengo hili kwa sasa umefikia asilimia 90 na mkandarasi anaendelea na kazi ili kukamilisha sehemu chache kabla ya kulikabidhi rasmi.

Amebainisha kuwa mradi huu umegharimu kiasi cha bilioni 40 na jengo litakuwa na mifumo mbalimbali ya Tehama itakayosaidia kufuatilia hali ya upatikanaji wa huduma kwenye maeneo yote ya kihuduma." amesema Ndugu Kingu.

DAWASA imehamisha baadhi ya ofisi zake ikiwemo Idara ya Fedha, Idara ya Tathmini, Ufuatiliaji na Mipango, Idara ya Uzalishaji na Usambazaji Maji, Idara ya Biashara na Kitengo cha Mawasiliano kutoka ofisi za awali zilizokuwa eneo la Gerezani (Sokoine drive).
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages