Breaking

Tuesday, 24 October 2023

Imbeju ya Benki ya CRDB yatoa mtaji wezeshi shilingi bilioni moja mpaka sasa



Newala. Tarehe 22 Oktoba 2023: Katika kuwafikia na kuwanufaisha zaidi wanawake wajasiriamali, CRDB Bank Foundation imeshiriki Mkutano Mkuu wa nne wa Mwaka wa BUT Vicoba uliowakutanisha zaidi wanachama 3,500 kutoka vikundi 318 vilivyoshiriki na kutoa mtaji wezeshi wa fedha taslimu na pikipiki.

Akizungumza na wanachama hao, Mkurugenzi Mtandaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa kwa hamasa aliyoiona ameamini kuwa kweli BUTA Vicoba ni taasisi kubwa yenye uwakilishi nchi nzima jambo linaloleta matumaini ya kulikomboa kiuchumi kundi hilo.

Tully amesema ni jambo la kujivunia kuona wanawake wanakusanyika kwa pamoja kupanga maendeleo ya uchumi wao binafsi na wa familia zao jambo litakalowaongezea ushiriki wao kwenye uchumi wa taifa letu.
“Leo tunakabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 20 pamoja na pikipiki 5 zenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa wana BUTA Vicoba. Huu ni mtaji wezeshi kwa baadhi yenu waliokidhi vigezo. Lengo la kuanzishwa kwa CDRB Bank Foundation ni kuwahudumia Watanzania hasa makundi yasiyopewa kipaumbele na taasisi nyingi za fedha nchini ambayo ni wanawake na vijana. Mliopata mtaji huu wezeshi leo mnaungana na wenzenu ambao tayari tumeshatoa shilingi bilioni 1 kwao,” amesema Tully.


CRDB Bank Foudation ni kampuni tanzu ya Benki ya CRDB iliyoanzishwa na kusajiliwa mwaka 2022 kwa lengo mahsusi la kuwawezesha vijana na wanawake. Kwa sasa taasisi hii inatekeleza Programu ya Imbeju iliyotengewa bajeti ya kuanzia kiasi cha shilingi bilioni 5 kwa ajili ya makundi hayo.


Ili kuyafikia makundi hayo kirahisi, inashirikiana na wadau muhimu wenye mtandao mpana. Kwa vijana wenye bunifu za kiteknolojia (startups), taasisi inashirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Tume ya TEHAMA (ICTC) na kwa wanawake wajasiriamali kuna BUTA Vicoba, Shirika la Care International, Citizen Foundation na wengine.
Tangu Programu ya Imbeju ilipozinduliwa Machi 12 mwaka huu, vijana 709 walijitokeza kutuma maombi ambayo yalipochujwa, miradi 196 ilikubaliwa na kuingia hatua ya mafunzo ya kujengewa uwezo wa kuendesha biashara kwa viwango vinavyofaa ndani ya nchi na kimataifa.


Bunifu 51 kati ya 196 zilikidhi vigezo vya kuendelea na tayari baadhi ya vijana wakundi hili wameanza kupewa mtaji wezeshi ili kukuza miradi yao.


Kuhusu mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha, Tully amesema makundi yote mawili yanapata na mpaka sasa tayari zaidi ya wajasiriamali 100,000 wamefunzwa; wanawake kwa wanaume.


“Tunapowawezesha wanawake na vijana, naomba nieleweke kuwa tunaangazia wanawake na vijana waliopo kwenye vikundi, vile vilivyosajiliwa na ambavyo vimefanya kazi walau kwa miaka mitatu mpaka sasa na lazima viingie mkataba wa makubaliano (Memorandum of Understanding) na CRDB Bank Foundation na kikundi kiwe na akaunti Benki ya CRDB.

Vikundi ambavyo havijakidhi vigezo hivi pia vinakaribishwa kujiunga kwani watapewa mafunzo ambayo yatawakuza na kuwawezesha kunufaika na Programu ya Imbeju huko mbeleni,” amesema Tully.


Tully pia aliitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa BUTA Vicoba, Semeni Gama kwa jinsi anavyojiyoa kuhakikisha wananchi wanachakarika nchini ili kujikwamua kiuchumi.


“Katika safari hii ya mafanikio tunao watu vinara waliotushika mkono sisi CRDB Bank Foundation na Programu ya Imbeju. Vinara hawa wanaongozwa na Mama Semeni. Sisi tunamwita mwamba kwani amekuwa na mchango mkubwa kwenye idadi ya wanawake tuliowapa mafunzo na wale waliofungua Akaunti ya Imbeju.

CRDB Bank Foundation tunampongeza Mama Semeni kwa jinsi anavyojitoa kwa ajili ya maendeleo na mafanikio ya wanawake wenzake. Tukiwa na watu wengi kama hawa wasiotulia mpaka waone wenzao nao wanachakarika, nina uhakika tutafanikiwa kukabiliana na umasikini unaozisumbua kaya zetu nyingi hapa nchini,” amesema Tully.


Kwa upande wake, Semeni ameishukuru Benki ya CRDB kupitia taasisi yake ya CRDB Bank Foundation kwa jinsi ilivyojitoa kuwawezesha wanawake ambao wengi hawapewi nafasi kwenye taasisi nyingi za fedha kutokana na kutokidhi vigezo vilivyowekwa.


“Ili kupata mkopo kwenye taasisi nyingi za fedha nchini, mteja anahitaji kuwa na dhamana lakini wanawake wengi hawamiliki ardhi kutokana na mila zilizopo maeneo mengi. Programu ya Imbeju ambayo imeondoa kigezo hicho inawafaa wanawake wengi watakaoweza kuanzisha biashara zao hivyo kujiingizia kipato cha uhakika,” amesema Semeni.










;

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages