Breaking

Monday, 2 October 2023

HOSPITALI ZA HALMASHAURI ZAPEWA MIEZI SITA KUPIMA SIKOSELI KWA WATOTO



Na. WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amezitaka Hospitali zote za Halmashauri nchini kuwapima ugonjwa wa Sikoseli watoto wote wanaozaliwa katika Hospitali hizo ili kujua Hali zao mapema na kuanza matibabu.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Octoba 2,2023 wakati akizindua kampeni ya kuelimisha jamii juu ya Magonjwa Yasiyoambukiza yaliyofanyika katika Hospitali ya Sinza - Palestina Jijini Dar es Salaam.

“Waganga Wakuu wa Mikoa mkalisimamie hili nataka Hospitali zote za Halmashauri nchini ndani ya Miezi Sita zipime ugonjwa wa Sikoseli kwa watoto wanaozaliwa katika Hospitali hizo kabla sijashuka vituo vya Afya”. Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 70 hadi 90 ya watoto wanaozaliwa na Sikoseli hupoteza maisha ndani ya kipindi cha Miaka Mitano ya mwanzo wa maisha yao kutokana na kutotambulika au kwa sababu ya unyanyapaa na kukosa elimu.

“Hali hii haikubaliki ni lazima tuchukue hatua za haraka ili kuokoa maisha ya watoto wachanga wenye ugonjwa wa Sikoseli kwa kuwatambua mapema ili kuhakikisha wanapata matibabu kwa wakati.

Waziri Ummy amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa fedha za dawa kwa asilimia 100 kila mwezi, fedha hizo wanaruhusiwa kuzitumia kwa ajili ya kununua mashine za kupima ugonjwa wa Sikoseli.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amesema ugonjwa wa Saratani umeongezeka kwa kasi Mwaka 2020 ambapo umeonesha vifo vipya zaidi ya Elfu 40 na vifo Elfu 26,945 ikiongozwa na Saratani ya Mlango wa Kizazi, tusipochukua tahadhari ugonjwa wa Saratani unaweza kufikia vifo Mil. Moja ifikapo Mwaka 2050

Akiendelea kufaganua kuhusiana na magonjwa Yasiyoambukiza, amesema magonjwa hayo ikiwemo Saratani yanachangia kwa asilimia 33 ya vifo vyote nchini Tanzania.

“Kwa upande wa nchi yetu takwimu zinaonesha magonjwa hayo yameongezeka kwa mara Tano hadi Tisa zaidi kati ya miaka ya 80 ambapo asilimia Moja tu ya Watanzania walikua na tatizo la Kisukari na 5% walikua na tatizo la Shinikizo la juu la Damu na sasa Kisukari 9% na Shinikizo la Damu 25%”. Amesema Waziri Ummy

Ili kupunguza tatizo la magonjwa Yasiyoambukiza, Waziri Ummy amewataka Watanzania kupunguza matumizi ya pombe kwa kuwa imekuwa sababu ya kuongezeka kwa magonjwa hayo nchini.

“Takwimu za mwaka 2023 zinaonesha ongezeko la matumizi ya pombe hadi kufikia matumizi ya wastani wa lita 10.4 kwa mwaka kwa watu wote wenye umri zaidi ya miaka 15 ambapo zinaiweka Tanzania kuwa nchi ya Tatu kwa matumizi ya Pombe”. Amesema Waziri Ummy

Mwisho, Waziri Ummy amesema takwimu za Ugonjwa wa Afya ya Akili zinaonesha kuwa wastani wa mtu Mmoja kati ya watu Wanne Duniani hupata maradhi ya Afya ya Akili kwenye maisha ambayo pia huchangia 21% ya ulemavu kwa mwaka.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages