Wafanyakazi wakiwa katika kikao kabla ya kuanza majukumu kwenye Kambi ya muda ya utafutaji mafuta Bukundi
Meneja mradi wa utafutaji wa mfuta bonde la Eyasi Wembere Mjiofizikia Sindi Maduhu akitoa elimu ya mradi kwa wananchi.
****
Mradi wa utafutaji mafuta na gesi asilia katika kitalu cha Eyasi Wembere ni miongoni mwa miradi ya kielelezo ya Taifa (flagship projects) ambao umeainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (Five Year Development Plan 2021 hadi 2026) inayotekelezwa na Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania. Mradi huu unatekelezwa katika eneo la Eyasi Wembere lililopo katika bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki likijumuisha mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu na Arusha.
Shughuli za utafutaji wa mafuta katika eneo hili zilianza mnamo mwaka 2015, ambapo taarifa zenye urefu wa takribani kilomita 11,323 za uzani na usumaku zilichukuliwa pamoja na taarifa za kijiolojia za miamba, uchorongaji wa visima vifupi vitatu kwa ajili ya kutambua miamba yenye viashiria vya uwepo wa Mafuta/Gesi Asilia. Visima hivi vifupi vya utafutaji wa miamba vilichorongwa katika maeneo ya Kinig’inila (Igunga), Luono (Iramba) na Nyalanja (Meatu), kutengeneza moduli ya data kani (gravity model), na kuandaa mpango wa uchukuaji wa takwimu za awali za mitetemo. Aliongea Sindi
Aidha ilielezwa kuwa, katika mwaka wa fedha 2022/23, Shirika lilikamilisha shughuli za uchukuaji na utafsiri wa takwimu za kijiokemia ambazo zimeleta matokeo chanya ya uwezekano wa uwepo wa viashiria vya miamba yenye uwezo wa kuzalisha mafuta au gesi asilia.
Wananchi waliohudhuria mkutano wakiangalia kifaa cha kukusanya taarifa za mitetemo kijulikancaho kwa jina la ‘Stryde Node’
Kufuatia shughuli hizo, Shirika limeendelea kutekeleza mkakati wa kuelimisha wananchi wanaoguswa na mradi huo kwenye mikoa yote mitano na wilaya sita za Karatu, Igunga, Meatu, Mkalama, Iramba na Kishapu kwa lengo la kuwajengea uwezo wananchi kuelewa shuhghuli za mradi, ulinzi na usalama na kutambua fursa zinazoambatana na mradi huo.
Akiongea na wananchi katika kijiji cha Kining’inila kilichopo wilaya ya Igunga Mjiofizikia Sindi Maduhu aliwaeleza wananchi kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/24, Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni nane (8) ili kukamilisha hatua za awali za utafutaji wa mafuta kwa njia ya mitetemo ya mfumo wa 2D, hivyo alitoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalmu watakaokuwa wakipita katika maeneo yao ili zoezi hili likamilike kwa wakati. Hata hivyo aliwaeleza wananchi kutokua na hofu wala woga pindi wataalamu wa utafutaji watakapofika kwenye maeneo yao kwani tafiti hizi huambatana na kuwepo kwa kifaa cha kurekodia mitetemo vinavyoitwa ‘Node’ na magari makubwa ambayo hutumika kuzalisha mitetemo na hataye kupata taarifa za miamba.
Magari maalumu ya utafutaji wa mafuta yakiwa yamejipanga tayari kwa ajili ya kupiga mitetemo ili kukukusanya taarifa za uwepo wa mafuta(2D data acquisition) katika kijiji cha Mwambagimu Wilaya ya Meatu.
Aidha, katika kijiji cha Isakamaliwa kilichopo kata ya Isakamaliwa –Igunga Afisa Maendeleo ya Jamii wa TPDC Bw. Oscar Mwakasege alisisitiza wananchi kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa mali za wakandarasi wakati wa shughuli za utafutaji wa mafuta. Katika kuongeza wigo wa utoaji elimu shule mbalimbali zilifikiwa kupatiwa elimu. Hatua ya kuwafikia wanafunzi ni muhimu sana kwani wanafunzi wakiwa na uelewa watafikisha ujumbe kwa ndugu, jamaa na jamii kwa ujumla kwa idadi kubwa.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Isakamaliwa iliyopo kijiji cha Sakamaliwa-Igunga wakipatiwa elimu ya utafutaji wa mafuta
Wanafunzi wa shule ya Msingi Kidalu Wilayani Igunga wakiwa wameshika picha zinazoonesha vifaa vya utafutaji wa mafutawakati wa zoezi la utoaji elimu.
Akiongea katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, Mwenyekiti wa kijiji cha Kinging’inila ndugu Christopher Zengwe ametoa rai kwa wananachi kushirkiana kuulinda mradi ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa watafiti pamoja na kuchangamkia fursa zitakazoambatana na mradi huo kama ajira za muda mfupi na muda mrefu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kining'inila Ndg.Christopher Zengwe akieleza jambo kwa wananchi wakati wa zoezi la utoaji elimu kijijini hapo.
Katika hatua nyingine Mbunge wa Jimbo la Meatu-CCM Mhe.Leah Komanya alipongeza jitihada zinazofanywa na TPDC katika kutafuta mafuta nchini na aliongeza kuwa serikali ya Chama cha Mapinduzi inatambua umuhimu wa kujenga uchumi wa kitaifa ili kuhakikisha kwamba Watanzania ndio wanufaika wakuu wa fursa za kiuchumi zinazotokana na rasilimali za nchi. Kwa muktadha huo serikali imeendelea na juhudi za kuifanya Tanzania kuwa nchi inayojitegemea kiuchumi pamoja na kuhakikisha rasilimali za asili za nchi hii kama gesi asilia zinanufaisha wananchi na Taifa kikamilifu.
Mbunge wa Jimbo la Meatu Mhe.Leah Komanya akifafanua jambo wakati wa zoezi la utoaji elimu kwa jamii katika kijiji cha Ng’wabalebi Wilayani Meatu
Akielezea ushiriki wa wazawa kwenye mradi, Sindi alisema kuwa katika hatua hii ya ukusanyaji wa data za mitetemo, mradi umechangia kutoa ajira kwa watanzania ambapo zaidi ya ajira 250 zimetolewa.
Steve Wawa yeye ni mnufaika wa ajira katika kambi ya muda ya utafutaji mafuta iliyopo kijiji cha Bukundi wilayani Meatu alisema mradi umemsaidia kupata fedha za kutimiza mahitaji ya familia yake pamoja na kuendesha maisha ya kila siku ikiwa ni pamoja kusomesha watoto wake.
Aidha, Meneja Mradi Sindi aliongeza kuwa, Shirika limeshaingia mkataba na mkandarasi African Geophysical Services-(AGS) kwa ajili ya kukusanya na kuchakata taarifa za mitetemo ya mfumo wa 2D kiasi cha urefu wa kilomita 260 ili kuwezesha kupata taarifa za uwepo wa miamba tabaka pamoja mashapo yatakayokuwa na uwezekano wa kuwa na Mafuta/ Gesi Asilia. Kampuni hii imeweka kambi ya muda katika kijiji cha Bukundi wilaya ya Meatu kwa ajili ya muda ili kutekeleza shughuli za kukusanya taarifa za mitetemo kwa kushirikiana na TPDC.
Muonekano wa Kambi ya muda ya utafutaji wa mafuta iliyopo kijiji cha Bukundi-Meatu
Kaimu Meneja wa mradi wa uchukuaji taarifa za Mitetemo wa kampuni ya AGS Ayman Abdeltawab alieleza kuwa katika kutekeleza dhana ya uwajibikaji wa Kampuni kwa jamii, kampuni inatarajia kuinua huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo upatikanaji wa maji safi kwa kuchimba visima vya maji vitatu (3) katika maeneo ya shule ya msingi Bukundi, Kituo cha Afya pamoja na eneo la kijiji.
Uchimbaji wa kisima cha maji katika eneo la kambi ya muda iliyopo kijiji cha Bukundi-Meatu
Akieleza faida za mradi Sindi aliongeza kuwa, utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuchangia upatikanaji wa nishati ya mafuta nchini na kuongeza kipato kwa nchi pale itakapouzwa kama malighafi nje ya nchi. Mradi huu umepitiwa na bomba la mafuta litokalo Uganda jambo ambalo litapunguza gharama za uendelezaji wa kitalu hiki na hivyo kuongeza faida kwa Taifa. Mradi huu pia utaendelea kutoa ajira kwa kuwapa kipaumbele watanzania katika kipindi chote cha utekelezaji wake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Athuman Hamisi Masasi alipotembelea kambi ya shughuli za utafutaji wa mafuta iliyopo katika kijiji cha Bukundi ili kujionea kazi zinazofanyika ambapo aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha Utafutaji unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
#TPDCTUNAWEZESHA.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Ndugu. Athuman Hamisi Masasi (kushoto) akiongea na wataalamu wa mradi mara alipotembelea kwenye kambi ya muda ya shughuli za utafiti iliyopo kjiji cha Bukundi Wilayani Meatu