Breaking

Monday, 9 October 2023

DAWASA YATETA NA WAKAZI MWEMBE BAMIA



Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam kupitia mkoa wa kihuduma DAWASA Mbagala imetoa elimu ya huduma za majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi wa Mwembe Bamia, Kata ya Chamazi wilayani Temeke ambao ni wanufaika wa huduma za Mamlaka.

Akizungumza katika mkutano huo, Afisa huduma kwa wateja Bi. Safina Mukhi amefafanua gharama na njia za malipo kwa wateja wanaohitaji huduma ya maji gharama kuwa hupatikana baada ya mteja kuwa ameshafanyiwa utafiti (survey) na kupewa gharama za vifaa ambazo zitalipiwa kupitia kumbukumbu namba atakayopatiwa.

"Gharama za maunganisho ya huduma kwa mteja baada ya kufanya tafiti (survey) kutoka kwenye bomba kuu hadi makazi ya mteja kupitia line ndogo zilizowekwa (line extension). Hivyo sio rahisi kukadiria gharama pasipo kufanyiwa survey." amesema Bi. Safina.

Ameongeza kuwa umbali ulioainishwa na EWURA na unaotekelezwa na Mamlaka ni kuanzia mita 50 kutoka lilipo bomba kuu.

"Kwa kawaida hizi gharama za maunganisho kwa kila mteja haziwezi kufanana na mwingine kutokana na umbali kwa kuwa aliyeko mita 50 atapata gharama tofauti na mkazi aliyepo mita 30 au 40." ameeleza Bi. Safina.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mwembe bamia Ndugu Abeid Miele ameishukuru DAWASA kwa kushiriki mkutano na kuzungumza na wananchi waliokuwa na shauku ya kusikia taarifa mbalimbali za DAWASA.

"Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa dhati DAWASA kwa kukubali kushiriki kwenye mkutano huu pamoja na kufafanua mambo mengi ambayo tulikuwa na maswali nayo, elimu iliyotolewa imesaidia kujua mambo mengi yaliyokuwa hususani taratibu za kupata maunganisho mapya ya huduma." amesema Ndugu Kindamba.

Nae Bi. Aisha Zuberi mkazi wa Mwembe bamia ameishukuru DAWASA kwa kutolea ufafanuzi wa gharama maunganisho ya maji pamoja na elimu ya huduma mbalimbali zitolewazo na DAWASA.

"Tunawashukuru sana DAWASA kutupa elimu juu ya mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kupata maji na ufafanuzi kuhusu mita 50, hii ni elimu tosha na ya muhimu sana," amesema Bi Aisha.

Kupitia mkutano huo, DAWASA imetoa elimu ya utunzaji wa maji, hifadhi za Mazingira na namna ya kuwasiliana na Mamlaka kupitia mawasiliano rasmi ya Mamlaka.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages