Breaking

Thursday 5 October 2023

DAWASA YAGONGA HODI KWA WANANCHI MAKONGO WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA



Wiki ya huduma kwa mteja ikiwa inaendelea, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imetembelea wateja wake katika eneo la Makongo wilayani Ubungo kwa lengo la kubadilishana nao mawazo juu ya uboreshaji huduma za maji

Akizungumza na wateja mbalimbali, Mkurugenzi wa Biashara (DAWASA) CPA (T) Rithamary Lwabulinda ameahidi kuendeleza mashirikino mazuri yaliyopo baina ya Mamlaka na wateja ili kuhakikisha huduma bora inawafikia wote kwa wakati.

"Leo tumewatembelea wateja mbalimbali ikiwemo Chuo Cha Ardhi ambao Mamlaka tunatekeleza mradi wa kuongeza huduma ya maji katika mradi wao wa majengo ya chuo unaoendelea. Tumewahaidi ifikapo tarehe 7, Oktoba 2023 huduma ya maji itakua imeanza imefika eneo la ujenzi. " ameeleza ndugu Lwabulinda.

Lwabulinda ameongeza kuwa Mamlaka imejipanga kuongeza maunganisho ya huduma ya maji na kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa huduma ifikapo mwaka 2025.

"Tumeadhimisha wiki ya huduma kwa wateja kwa kutembelea wateja wakubwa na wadogo, tunafahamu kuna maeneo ambayo bado huduma haijafika, nipende kuwahakikishia wananchi kuwa Mamlaka inafanya kazi kubwa kusogeza huduma maeneo yote kwa kuongeza vyanzo vya maji na kufanya miradi ili kila mwananchi apate huduma ya maji" ameeleza ndugu Lwabulinda.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Profesa Evaristo Liwa ameishukuru DAWASA kwa huduma bora zinazotolewa chuoni hapo na kuahidi ushirikiano wa kutosha baina ya Chuo na DAWASA.

"Nikiri kwamba DAWASA wanatoa huduma bora hapa kwetu, huduma ya maji tunaipata kama inavyostahiki na imechangia utulivu mkubwa kwa wanafunzi chuoni hapa, tutaendelea kutoa ushirikiano kwao Ili huduma hii bora iwe endelevu" ameeleza Profesa Liwa.

Frida Jackson mkazi wa Makongo ameishukuru DAWASA kwa kuwafikia katika wiki hii ya huduma kwa mteja na kueleza kuridhishwa na huduma.

"Miaka ya nyuma eneo la Makongo kulikuwa na shida kubwa ya maji, lakini sasa huduma imeimarika sana, tunapata huduma saa 24, nitumie nafasi hii kuwasihi wananchi wenzangu kulipia huduma za maji kwa wakati ili na sisi tuweze kupata huduma bora kwa wakati"ameeleza ndugu Frida.

Wiki ya huduma kwa wateja inaakisi usimamizi bora na wa viwango wa huduma zitolewazo na Mamlaka kwa wateja na kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Huduma kwa Ushirikiano".


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages