Breaking

Thursday, 5 October 2023

DAWASA: UPATIKANAJI YA HUDUMA YA MAJISAFI KUFIKIA ASILIMIA 95 IFIKAPO 2025

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam, (DAWASA) imetembelea katika Chuo cha Ardhi na maeneo ya Makongo na kusikiliza maoni ya hutoaji huduma kwa wateja wao ikiwa wanaadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Biashara (DAWASA) CPA (T) Rithamary Lwabulinda amesema wamejipanga kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji unafikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.

Aidha ameahidi kuendeleza mashirikino mazuri yaliyopo baina ya Mamlaka na wateja ili kuhakikisha huduma bora inawafikia wote kwa wakati katika maeneo mengi.

"Tunafahamu kuna maeneo ambayo bado huduma haijafika, nipende kuwahakikishia wananchi kuwa Mamlaka inafanya kazi kubwa kusogeza huduma maeneo yote kwa kuongeza vyanzo vya maji na kufanya miradi ili kila mwananchi apate huduma ya maji". Amesema Lwabulinda.

Nae Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Prof. Evaristo Liwa ameishukuru DAWASA kwa kuhakikisha huduma ya Majisafi inapatikana kwa wakati katika maeneo ya Chuo kwani maji yamekuwa ni muhimu kwa kiasi kikubwa hivyo ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa DAWASA.

Kwa upande wa wananchi wa maeneo ya Makongo wamesema wamekuwa wakipata huduma ya majisafi kwa wakati na ikitokea kuna tatizo basi DAWASA huwa wanatoa taarifa kwa wakazi hao na baada ya muda maji yanaendelea kupatikana kama kawaida.

"Miaka ya nyuma eneo la Makongo kulikuwa na shida kubwa ya maji, lakini sasa huduma imeimarika sana, tunapata huduma saa 24, nitumie nafasi hii kuwasihi wananchi wenzangu kulipia huduma za maji kwa wakati ili na sisi tuweze kupata huduma bora kwa wakati"amesema Bi. Frida Jackson mmoja wa wakazi wa Makongo Ubungo Jijini Dar es Salaam.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages