Katika mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa Elimu ya Juu Kwa Mageuzi ya Kiuchumi “HEET – Project” Chuo Kikuu Mzumbe kimesaini mkataba na Kampuni ya “Y & P Architect” kwa ajili ya kutoa Huduma ya Ushauri wa Kitaalamu kwa ajili ya Usanifu na Usimamizi wa Miundombinu Mipya Chuoni hapo - Kampasi Kuu kupitia mradi wa HEET katika hafla iliyofanyika imefanyika Oktoba 09, 2023 Chuo Kikuu Mzumbe kampasi Kuu.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mratibu wa Mradi wa HEET, Dkt. Eliza Mwakasangula amesema hatua hii ni mwendelezo mzuri wa kuhakikisha mradi wa HEET unakamilika kwa ufanisi kama yalivyo malengo ya mradi na Taifa kwa ujumla.
Aidha Bw. Leonard Prosper, Mratibu wa Mradi wa HEET upande wa Miundombinu amebainisha baadhi ya maeneo ambayo kampuni ya “Y & P Architect” itashughulika nayo kupitia mkataba huu kuwa ni pamoja na Usanifu wa majengo, Barabara za ndani, Mifumo ya majitaka na Majisafi na Uboreshaji wa miundombinu ikiwemo michezo. Pia Mshauri wa Kitaalamu atapaswa kuwasilisha taarifa ya kazi zake ambayo itapitiwa na Kamati ya Menejimeti ya Chuo kwa ajili ya kujiridhisha na hivyo kutoa nafasi ya kutangaza kandarasi kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa miundombinu tajwa.
Kwa upande wake Prof. William Mwegoha, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, ameishukuru Serikali kwa mradi ambao una tija kwa Chuo; kwakuwa kupitia mradi huo wa HEET, Chuo Kikuu Mzumbe kimepewa Dola za Kimarekani Milioni 21, na asilimia 78 ya pesa hizo zimeelekezwa katika kuboresha miundombinu, na ndio sehemu ya mkataba uliosainiwa.
Ameipongeza Kampuni ya “Y & P Architect” kwa kupata nafasi ya kufanya kazi na Chuo Kikuu Mzumbe hasa katika utekelezaji wa mradi wa kimkakati. Prof. Mwegoha ameitaka kampuni hiyo kufanya kazi kwa weledi mkubwa kwakuzingatia zaidi ubora na muda ambao kazi hiyo inapaswa kuwa imekamilika.
Pia amesisitiza na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano na ufatiliaji wa kila hatua ya kazi itakayofanyika ili kubaini na kutatua changamoto zitakazojitokeza.
Akizungumza Katika hafla hiyo ya uwekaji Saini mkataba huo, Mhandisi. Yasin Mringo, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya “Y & P Architect” amekishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa kutoa fursa ya kufanya kazi kwa pamoja katika kutekeleza mradi wa HEET. Mhandisi Mringo ameahidi kutekeleza majukumu aliyopewa kwa weledi, ubora na ufanisi mkubwa ili kufikia malengo yao kama kampuni lakini pia kusaidia malengo ya Chuo Kikuu Mzumbe na Serikali kwa ujumla huku akisisitiza kuwa kampuni yao inawataalamu wa kutosha kukamilisha kazi kama ilivyopangwa.
Katika kuhitimishwa kwa hafla hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Mipango, Fedha na Utawala Prof. Allen Mushi ametoa neno la shukrani kwa menejimenti ya Chuo,waratibu wa Mradi wa HEET na kampuni ya “Y & P Architect” kwa kusaini mkataba. Prof. Mushi amesema kuwa shauku ya menejimenti ni kuona hatua ya awali inakamilika mapema ili kutoa nafasi kwa Mkandarasi kuanza kazi mapema.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Y & P Architect Mhandisi Yasin Mringo (kushoto) wakisaini Mkataba wa Kutoa Huduma ya Ushauri wa Kitaalamu wa Usanifu na Usimamizi wa Miundombinu Mipya Chuo Kikuu Mzumbe (Kampasi Kuu) chini ya Mradi wa HEET. Kulia ni Mwanasheria wa Chuo na Kaimu Katibu wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Bi. Eveline Kweka. Hafla hiyo ya utiaji saini mkataba tajwa imefanyika tarehe 09.10.2023 katika viunga vya Chuo Kikuu Mzumbe.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha (kulia) akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa hafla ya kusaini Mkataba wa Kutoa Huduma ya Ushauri wa Kitaalamu wa Usanifu na Usimamizi wa Miundombinu Mipya Chuo Kikuu Mzumbe (Kampasi Kuu) chini ya Mradi wa HEET. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Y & P Architect (iliyoshinda zabuni) Mhandisi Yasin Mringo. Hafla hiyo imefanyika tarehe 09.10.2023 katika viunga vya Chuo Kikuu Mzumbe huku ikihudhuriwa na viongozi kadhaa wa Menejimenti ya Chuo hicho.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Y & P Architect, Mhandisi Yasin Mringo (kushoto) wakiwa wameshika nakala za Mkataba wa Kutoa Huduma ya Ushauri wa Kitaalamu wa Usanifu na Usimamizi wa Miundombinu Mipya Chuo Kikuu Mzumbe (Kampasi Kuu) chini ya Mradi wa HEET baada ya pande zote mbili kusaini mkataba huo. Hafla hii ya utiaji wa saini mkataba tajwa imefanyika tarehe 09.10.2023.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Y & P Architect Mhandisi Yasin Mringo (kushoto) wakikabidhiana Mkataba wa Kutoa Huduma ya Ushauri wa Kitaalamu wa Usanifu na Usimamizi wa Miundombinu Mipya Chuo Kikuu Mzumbe (Kampasi Kuu) chini ya Mradi wa HEET baada ya kusaini mkataba huo.