Breaking

Thursday, 5 October 2023

CHONGOLO: MAWAZIRI 3 KUHUSIKA FIDIA MRADI WA UMEME TABORA - KATAVI

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema atakutana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Nishati na Wizara ya Fedha, kwa ajili ya kutatua changamoto ya malipo ya fidia ya wananchi ambao ardhi yao imechukuliwa kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Msongo wa Umeme kutoka Tabora hadi Katavi.

Katibu Mkuu Ndugu Chongolo amesema hayo leo Oktoba 5, 2023, wakati akizungumza na wananchi wa Inyonga, wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi, kuhusu mradi huo wa msongo wa umeme ambao utauwezesha mkoa huo sasa kuunganishwa katika gridi ya taifa, hivyo kumaliza kabisa changamoto ya nishati hiyo katika maeneo hayo.

“Nikirudi Dar es Salaam nitakaa na pande zote zinazohusiana na ulipaji fidia wakiwemo Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na Wizara ya Ardhi pamoja na wadau wengine ili watuambie wanaendaje na nini kifanyike kusukuma suala la fidia ili walipwe haraka.

Ndugu Chongolo amewahikishia wananchi wa Mkoa wa Katavi kuwa katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025, kuunganisha Mkoa wa Katavi kwenye gridi ya taifa, ni mojawapo ya vipaumbele vya muhimu kwa Serikali.

Chongolo ambaye yupo katika mkoa huo kwa ziara ya kuhamaisha uhai wa Chama, kukagua utekelezaji wa Ilani pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitafutia majawabu, amesema Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

“Na huu mradi sio mradi tu bali ni mradi wenye lengo mahususi la kutafuta majawabu kwa wananchi wa Katavi lakini pia kuinua shughuli za uchumi wao na wakazi wa jirani kama Sikonge na maeneo mengine.

“Mmeeleza vizuri uwezo wa kituo hapa ni megawati 1.4 na mahitaji sasa hivi yaweza kuwa yamefika megawati mbili lakini ukipeleka Majimoto kuna viwanda zaidi ya 20 au 30 vya mpunga vile viwanda vyote vinahitaji umeme.

“Ukipiga hesabu utakuta Majimoto nao wanahitaji megawati mbili mpaka tatu, kwa hiyo zinahitajika karibia megawati tano kwa wilaya ya Mlele. Ukienda Mpanda shughuli zao zinaunganisha mpaka Kalema na kalema tuna bandari." Amesema.

Ameongeza ili kubadilisha kwenda kwenye uhalisia ni kutekeleza huo mradi huku akitumia nafasi hiyo kuzungumzia suala la fidia kwa watakaopitisha mradi huo.

“Nikirudi Dar es Salaam nitakaa na pande zote zinazohusiana na ulipaji fidia wakiwemo Wizara ya Nishati,Wizara ya Fedha na Wizara ya Ardhi pamoja na wadau wengine ili watuambie wanaendaje na nini kifanyike kusukuma suala la fidia ili walipwe haraka.

Ameongeza fidia ikishalipwa itabaki kusubiri ujenzi wa laini ya umeme na kushauri watekelezaji wa mradi huo kuanzia shughuli za za awali za utekelezaji wa mradi huo kwa kuandaa mazingira.

“Wakati huu ungekuwa wakati muafaka wa kuanza kujenga nguzo kwenye maeneo yale yenye majimaji ili wakati wa masika ujenzi usimame maeneo hayo.Tunaomba mradi huu uangaliwe kwa uzito wake.

“Tukifungua na kuleta umeme kwa wananchi wa Katavi naamini mchango wao katika kukuza uchumi wa nchi hii utakwenda juu kwani kwa sasa hata ujenzi wa viwanda vikiwemo vya kuchakata tumbaku na migodi ya madini, umesimama kwasababu ya changamoto ya umeme,” amesema Ndugu Chongolo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages