Serikali imelitaka Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuhakikisha linapanga mikakati madhubuti itakaloliwezewesha kukua na kujiendesha kwa tija baada ya uwekezaji mkubwa unaofanywa kupitia ununuzi wa ndege za masafa mafupi, ya kati na marefu.
Akizungumza wakati akifungua Kikao cha Tano cha Baraza la Pili la Wafanyakazi mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Uchukuzi Lucas Kambelenje ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema ununuzi wa ndege hizo unaofanywa pamoja na maboresho katika viwanja unatarajiwa kuongeza tija katika usafiri wa anga nchini.
“Kama Serikali tunategemea ndege hizi 14 zilizonunuliwa ziwe na matokeo chanya ambayo yataonekana na niwahakikishie kuwa ndege zilizobaki Serikali itahakikisha zinakuja ili Shirika liendelee kupiga hatua”, amesema Kambelenje.
Mkurugenzi Kambelenje ameipongeza ATCL kwa kuhakikisha inapunguza gharama za uendeshaji kwa kuwawezesha wataalam wao kufanya matengenezo ya ndege wenyewe ili kupunguza utegemezi wa makampuni ya nje hadi kiwango cha matengenezo makubwa (C Check) hapa nchini na hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingelipwa kwa makampuni ya nje ya nchi,
Aidha, Kambelenje ameitaka ATCL kuhakikisha inaboresha huduma kwa wateja ili kuvutia wateja wengi zaidi kutumia Shirika hilo kwa safari za ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema ATCL imeweza kuweka mifumo mbalimbali inayowezesha mauzo kufanyika vizuri pamoja kuingia makubaliano na mashirika mengine ya kimataifa ili kupata wateja kwenye maeneo ambayo ATCL haitoi huduma.
Mwenyekiti Matindi ameongeza pamoja na mafanikio mengine ATCL kupitia Kitengo cha TEHAMA imeendelea kubuni mifumo mbalimbali ili kupunguza gharama za uendeshaji wa Kampuni hii.
Amebainisha kwamba, ATCL imefanikiwa kuongeza vituo hadi kufikia vituo 15 vya ndani na 11 vya nje ya nchi.
Baraza la Wafanyakazi wa ATCL litakutana kwa siku mbili mkoani Morogoro ambapo pamoja na kufanya tathimini ya utendaji Shirika hili pia litajadili Mpango Mkakati wa Pili wa Miaka Mitano (Corporate Strategic Plan 2022/23 – 2026/27) wa Kampuni hiyo.