Breaking

Tuesday, 12 September 2023

WAZIRI AWESO AWAPA MAAGIZO DAWASA UPATIKANAJI HUDUMA YA MAJI MBAGALA

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kushirikiana na Bonde la Maji Wami Ruvu kufanya utafiti wa maeneo ya kuchimba visima kwenye Jimbo la Mbagala, wilayani Temeke ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya Majisafi kwa wananchi.

Pia ameitaka DAWASA kukamilisha utekelezaji wa mradi wa maji ndani ya wiki tatu kuanzia sasa ambao unaotekelezwa maeneo ya pembezoni mwa mji kwa ushirikiano na Benki ya Dunia ili wananchi Mbagala, wanufaike.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua upatikanaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya majisafi inayoendelea katika jimbo hilo.

Ameongeza kuwa wananchi wa Mbagala hususani Kata ya Chamazi wanauhitaji mkubwa wa huduma ya Majisafi, hivyo DAWASA inatakiwa kuongeza nguvu ya upatikanaji wa maji kupitia visima virefu pamoja na ukamilishaji wa miradi ili kuleta manufaa kwa wananchi.

"Niwatake kuongeza nguvu kwenye eneo la utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na kuhakikisha wateja walioomba huduma wanaunganishwa kwa wakati kulingana na mkataba wa huduma kwa wateja unavyotaka." amesisitiza Mhe. Aweso.

"Pia DAWASA ihakikishe inawekeza nguvu nyingi kwenye maeneo ambayo bado yana changamoto ya maji ikiwemo Jimbo la Ukonga, Chanika, Kibamba na Kinyerezi ili kuondoa malalamiko ya wananchi yanayoendelea sasa." ameeleza.

Mhe. Aweso amewakumbusha watumishi wa DAWASA kuwa na kauli nzuri wakati wa kutoa huduma kwa wateja ili kuboresha mahusiano mazuri na huduma bora.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Mobhare Matinyi amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia uhitaji wa huduma ya maji kwa kutoa kiasi cha Shilingi bilioni 15 kwa mwaka wa fedha uliopita 2022/23 ambazo zimesaidia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema kuwa Mamlaka imefanikiwa kufikisha huduma katika mitaa 52 kati ya mitaa 67 ya Mbagala.

Ameongeza kuwa kwa sasa Mamlaka inakamilisha utekelezaji wa mradi wa maji (WSSP II) unaotekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia ambao umefikia asilimia 98 sasa.

"Mradi huu utaboresha upatikanaji wa huduma kwenye maeneo ya Mianzini, Butiama, Mwanamtoti, Kisewe na Magengeni kwa wakazi takribani 93,820," ameeleza Mhandisi Mtindasi.

Mhandisi Mtindasi amesema kuwa kwa sasa kazi inaendelea ya kuimarisha huduma katika maeneo ya Tuangona na Kilungule.

Naye mkazi wa Mianzini Mwanaisha Kayenje ameishukuru DAWASA kwa jitihada zinazoendelea za kuboresha huduma na ameomba Mamlaka kuongeza nguvu katika kukamilisha mradi ili Wananchi waanze kupata huduma ya maji.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages