Breaking

Tuesday, 26 September 2023

TUTALETA UMEME VIJIJINI- DKT. BITEKO



Na Lilian Lundo na Veronica Simba

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema shauku ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona kila Mtanzania anapata umeme bila kujali aina ya nyumba aliyonayo, kwani kila Mtanzania anahitaji mwanga.

Mhe. Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 26, 2023 wakati wa hafla ya uwashaji umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Kijiji cha Ihako kilichopo Kata ya Katome, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

“Tutaleta umeme vijijini, hata kama wananchi hawana nyumba nzuri wanahitaji mwanga, hata kama wana nyumba za nyasi ambazo hazina tarazo wanahitaji mwanga. Watakapopata umeme watapata shauku ya kujenga nyumba nzuri,” amesema Mhe. Dkt. Biteko.

Amesema Serikali imeanza kusambaza umeme katika ngazi ya vijiji, na baada ya vijiji vyote kupata umeme itashuka katika vitongoji.

Aidha, ameiagiza REA kwenda vijijini na kuzungumza na wananchi ili kujua changamoto zao na kuzitatua,

“Nendeni kwa wananchi, nendeni vijijini zungumzeni na wanavijiji, tukaongee lugha zao, tunataka kuona shughuli za REA zikifanyika vijijini na sio mjini, kazi kubwa ya REA ni kupeleka umeme vijijini na sio mijini, hivyo tunataka kuwaona kazi zenu mkifanyia vijijini,” amesema Mhe. Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unalenga kupeleka umeme katika vijiji vyote ambavyo awali havikuwa na umeme, ambapo katika Mkoa wa Geita vijiji 62 na vitongoji vikubwa 65 vitapatiwa umeme kupitia mradi huo, hivyo kufanya jumla ya vijiji/vitongoji vitakavyopatiwa umeme kupitia mradi huu kuwa 127.

“Mkoa wa Geita una jumla ya vijiji 461 ambapo vijiji 399 sawa na asilimia 86.6 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya awali ikiwemo REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, REA Awamu ya Pili na REA Awamu ya Kwanza.

Wakala wa Nishati vijijini umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika mkoa wa Geita ikiwa na lengo la kuwapatia huduma za Nishati kwa wananchi ili kuboresha huduma za jamii na kuimarisha shughuli za kiuchumi,” amesema Mhandisi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages