Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila amewatoa hofu wananchi wa Dar es Salaam kuhusu hali ya upatikanaji wa maji na kusema huduma ya maji bado inaendelea kupatikana kama kawaida kwa kuzingatia kiasi cha maji kinachozalishwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) licha ya kuwepo kwa changamoto ya huduma ya umeme.
Ametoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar hususani kwa wakazi wa Tegeta A, Mivumoni na Mbezi Beach walionufaika na mradi wa usambazaji maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo.
"Leo tumekagua miundombinu ya matenki ya kuhifadhi na uzalishaji maji inayotoa huduma ya maji kwa wananchi, niwapongeze sana DAWASA kwa jitihada kubwa wanazofanya za kuhakikisha wanazalisha maji lita milioni 590 za maji kila siku zinazosambazwa kwa wananchi wanaowahudumia”. ameeleza
Amefafanua kuwa kazi inayofanyika kwa sasa ni kusambaza maji kwa kasi kwenye maeneo yote ambayo huduma haijafika, pamoja na maeneo ambayo miradi imekamilika ikiwemo mradi huu wa Makongo hadi Bagamoyo.
"Nipende kuwatangazia wana Dar es Salaam kuwa mpaka sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji bado iko imara tofauti na kipindi kama hiki kwa mwaka jana ambapo hali ya kiangazi ilisababisha ukosefu wa maji kwenye maeneo mengi, haya ni matokeo ya utunzaji mzuri wa vyanzo vya maji unaosaidia Mto Ruvu kuwa na maji muda wote," ameeleza Ndugu Chalamila.
Amesisitiza kuwa utunzaji wa vyanzo vya maji ni jambo muhimu kwa sasa na vizazi vijavyo, na kuwataka wananchi wote kuwa mabalozi wazuri wa utunzaji wa vyanzo vya maji, ili huduma ya maji iendelee kupatikana.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Ndugu Adam Ngalawa amesema kuwa ameipongeza Serikali kupitia DAWASA kwa kazi kubwa inayofanyika ya kutoa huduma ya majisafi kwa wananchi wote, kwa kuwa hadi sasa hapajatokea changamoto yoyote ya hali ya majisafi tofauti na kipindi cha nyuma.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa hakuna changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa sasa, bado uzalishaji wa maji uko vizuri na huduma inaendelea kupatikana.
"Kazi kubwa tunayoendelea kuitekeleza kwa sasa ni kusogeza huduma ya majisafi kwa wananchi kwa nguvu zote ili maeneo yote yaweze kupata huduma," amesema.
"Kwa mradi wa Makongo hadi Bagamoyo, tayari tumeshafanya maunganisho ya maji kwa wananchi 30,000 na tunalenga kuunganisha wananchi 50,000," amesema.