Breaking

Sunday, 10 September 2023

TUJENGE NIDHAMU YA WIZARA- WAZIRI SILAA

Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amewataka watumishi wa Wizara yake kuhakikisha wanawahudumia vizuri wananchi ili wajenge imani na serikali.

‘’Lazima tutengeneze ‘despline’ ya wizara kwa kuwahudumia vizuri wananchi, tukumbuke hapa tunafanya kazi ya watanzania kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan’’ alisema Waziri Silaa.

Akizungumza na watumishi wa Wizara ya Ardhi baada ya uzinduzi wa Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya Taarifa za Kijiografia, Waziri Silaa amesema, wakati wa kutekeleza majukumu, watumishi hao wakumbuke kuwa siyo kila mwananchi ana haki lakini wanao wajibu wa kutenda haki wakati wote wa utekelezaji majukumu.

‘’Mna wajibu wa kusimamia haki na kila mtu atolee maamuzi kwa kazi inayowasilishwa kwake na kama mwananchi hapaswi kupewa kiwanja aelezwe bayana kwa maandishi’’ alisema.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, wizara yake kwa sasa inakwenda kufanya maboresho yanayolenga kuleta tija ambapo amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kuwa tayari kwa maboresho hayo.

‘’Mtu anafuatilia hati kwa zaidi ya miezi mitatu hapo kuna ‘question mark’ hata kama ni urasimu utakuwa umepitiliza’’ alisema.

Amewaeleza waumishi wa Wizara hiyo kuwa, pamoja na kuelezwa mambo mengi ya wizara yake lakini ana haki ya kusikiliza na kubainisha kuwa, atazitumia siku mia moja kujifunza ili watakapokutana kwenye maeneo ya kazi ajue cha kufanya.

Kikao hicho cha Waziri Silaa na watumishi kimehusisha viongozi wa Wizara, baadhi ya watumishi kutoka Makao Makuu, Ofisi za Ardhi za Mikoa pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akizungumza na watumishi wa Wizara na Taasisi zilizokuwa chini ya wizara hiyo mara baada ya uzinduzi wa Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya Taarifa za Kijiografia tarehe 9 Septemba 2023 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Jerry Silaa na watumishi pamoja na Taasisi zilizo chini ya wizara tarehe 9 Septemba 2023 jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Ardhi Mhe. Jerry Silaa na watumishi wa Wizara na Taasisi zake tarehe 9 Septemba 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akizungumza na watumishi wa Wizara na Taasisi zilizokuwa chini ya wizara tarehe 9 Septemba 2023 mkoani Dodoma.
Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakiwa kwenye kikao na Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Jerry Silaa tarehe 9 Septemba 2023 jijini Dodoma.

(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages