Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia wawekezaji katika Sekta ya Madini kutoka nchi ya Korea ya Kusini kuwa Serikali imeimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuhakikisha kila muwekezaji anayekuja kuwekeza nchini anapata faida kutokana na uwekezaji wake.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo, Septemba 2, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika mkutano baina ya Serikali ya Tanzania chini ya Wizara ya Madini na ujumbe kutoka Korea Kusini uliojumuisha viongozi wa makampuni makubwa ya madini yanayohusika na mnyororo wa thamani wa uzalishaji betri za magari na kujadili kuhusu ushirikiano katika uendelezaji wa madini ya kimkakati nchini Tanzania.
Lengo la mkutano huo ni kujadili fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini na kuona namna ya kushirikiana katika kuzitumia fursa hizo ambapo kampuni hizo kutoka Korea ya Kusini ni yaliyoshiriki ni pamoja na Posco Holdings, Posco International,SK, Korea Zinc na LX International.
Aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kwa uwekezaji wao na itawawezesha kuwekeza mitaji yao.
“Sisi tuna madini na ninyi ndugu zetu Wakorea mna mitaji, twende tuunganishe nguvu kwa manufaa ya nchi zote.”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Alisema Serikali imeimarisha mazingira ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya usafirishaji kama barabara, ndege na nishati ya kutosha kwa ajili ya uendeshaji wa viwanda, lengo ikiwa ni kuhakikisha kila muwekezaji anayekuja anapata faida kutokana na uwekezaji wake.
“Ninapenda kuwahakikishia kuwa nchi yetu ni salama na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kila linalowezekana kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.” aliongeza Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde aliishukuru Serikali ya Korea Kusini kwa kuichagua Tanzania na kufanya mazungumzo kuhusu uwekezaji katika Sekta ya Madini na kutumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo kuja kuwekeza hapa nchini.
"Tanzania inaweka kipaumbele katika uchimbaji wa Madini Mkakati kwa kufanya tafiti za madini hayo ili kuendana na soko hilo duniani. Aidha miradi mbalimbali ya Madini Mkakati inaendelea kutekelezwa katika Sekta ya Madini ikiwemo ya Lindi Jumbo na Kabanga Nikeli", alisema Waziri Mavude.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini humo, Togolani Mavura alieleza kuwa ushirikiano kati ya Korea kusini na Tanzania unazidi kuimarika na imani yake kuwa mada zilizowasilishwa na wataalam kutoka Wizara ya Madini kuhusu fursa zilizopo zimeongozea uelewa juu ya sekta hiyo.
Pia, Mjumbe Maalum wa Rais wa Korea ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe huo kutoka Korea Kusini, Bw. Yoon Sang Jick aliishukuru Serikali ya Tanzania nakuahidi kuwa wataendelea kushirikiana nayo kuhakikisha malengo ya uwekezaji yanafanikiwa.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Watendaji Wakuu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade).