Breaking

Thursday, 14 September 2023

NAIBU WAZIRI KAPINGA AIHIMIZA TANESCO KUBORESHA UPATIKANAJI UMEME MTWARA NA LINDI



Naibu Waziri Kapinga amelihimiza Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania - TANESCO kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha mikoa ya Mtwara na Lindi inapata umeme wa kutosha.

Naibu Waziri Kapinga ameyasema hayo leo tarehe 14/09/2023 wakati alipotembelea Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa kutumia Gesi Asilia cha Mtwara.

Kituo hicho kina mitambo 13 yenye uwezo wa kuzalisha umeme MW 30.4 lakini kwa sasa kinazalisha MW 19 kutokana na mitambo mitatu kuwa katika Matengenezo na kinahudumia mikoa ya Mtwara na Lindi.

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga ametembelea kituo hicho ili kuangalia halisi hali ya mitambo na uzalishaji wa umeme kituoni hapo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi.

Naibu Waziri Kapinga amemuelekeza Meneja wa Kituo hicho cha Kuzalisha Umeme kwa kutumia Gesi Asilia cha Mtwara, kuhakikisha wanafanya jitihada za kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme mkoani humo ili kukidhi hamu ya wakazi wa mikoa ya Mtwara na Lindi ya kupatiwa umeme wa kutosha.

Naibu Waziri Kapinga amesema, jukumu kubwa walilonalo nikuhakikisha kuwa Watanzania wanapata Nishati ya Uhakika.

Amesema, katika uongozi wake, kwa kushirikiana na Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake atahakikisha, anamsadia ipasavyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Biteko kuhakikisha wanatimiza kiu ya Watanzania kupata Nishati ya Uhakika.

Naibu Waziri Kapinga ameongeza kuwa, ili azma hiyo itimie, wanahitaji kupatiwa ushirikiano kutoka kwa watumishi wa Wizara na Taasisi zake ili kwa pamoja kutekeleza mipango iliyowekwa ya kuwapatia Watanzania Nishati ya Uhakika ikiwezekana kuzidi lengo lililowekwa na Serikali kufikia 2025.

Naibu Waziri Kapinga amesema, mafanikio yake kiuongozi kwa kiasi kikubwa yatategemea ushirikiano mzuri wa Watumishi wa Wizara na Taasisi zake katika kufanya kazi kwa bidii, maarifa, moyo wa kujituma na kwa ushirikiano.

Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa kutumia Gesi Asilia cha Mtwara, Meneja wa Kituo hicho, Mha. Mtoba Kasika Biseko, ameahidi kuwa, watafanya kazi kwa moyo wa kujituma na watawapatia ushirikiano mzuri viongozi katika kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, aliambatana na Kamishna wa Umeme wa Wizara ya Nishati, Mha. Innocent Luoga, Naibu Mkurugenzi, Usambazaji Umeme wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania - TANESCO Mha. Athanasius Nangali na Meneja TANESCO Mkoa wa Mtwara Mha. Tawakali Rwahila.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages