Breaking

Saturday, 30 September 2023

MWALIMU NYERERE MARATHONI SASA KUWA LA KIMATAIFA


Na John Mapepele

Serikali imesema inakwenda kulifanya tukio la mbio za Mwalimu Nyerere Marathoni linalofanyika kila mwaka kuwa tukio la kudumu na la kimataifa kwa kushirikisha mataifa mbalimbali duniani ili kuenzi historia ya baba wa taifa na kufungua zao jipya na la kipekee la utalii wa michezo kupitia jina la Baba wa Taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe. Moses Kaegele wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki leo Septemba 30, 2023 wakati wa Kilele cha msimu wa pili wa mbio za Mwalimu Nyerere Marathoni katika kiwanja cha Mwenge wilayani Butiama.

Aidha, amesema ameipenda kaulimbiu ya marathoni ya mwaka huu inayosema “Kilometa za Kizalendo” kwa sababu mbio hizi ni kwa heshima ya Baba wa Taifa, Mwalimu, Julius Kambarage Nyerere ambaye aliishi na kuongoza nchi kizalendo na alihamasisha uzalendo katika jamii nzima ambapo pia aliyaunganisha makabila yote kwa lugha moja ya kiswahili.

Amesema mbali na kutangaza urithi na historia ya Baba wa Taifa, kipekee kwa mwaka huu 2023 mbio hizi zinalenga kukusanya fedha na vifaa kwa ajili ya kuandaa na kuweka onesho maalumu kwa watu wenye mahitaji maalum (wasioona na wenye uono hafifu) kwa kutumia matumizi ya sauti na nukta nundu katika Makumbusho ya Mwalimu Nyerere Butima

Amefafanua kuwa kwa kutambua umuhimu huo, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliamua kuandaa Mpango wa Miaka Kumi wa Kumuenzi na Kutangaza Urithi wa Mwl Nyerere (2022 – 2032).

“Lengo kuu la mpango huo ni kuthamini urithi wa Baba wa Taifa ambapo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kujenga uelewa juu ya umuhimu wa kuthamini, kukusanya, kuhifadhi, kuendeleza na kutangaza urithi wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.” Amesisitiza .

Amepongeza ubunifu uliotumika kwenye mbio hizi ambapo amesema mfumo uliotumika umeashiria historia ya mwalimu ambapo amefafanua kuwa waliokimbia umbali wa kilometa 13 wameashiria tarehe aliyozaliwa Baba wa Taifa, waliokimbia kilometa 4 wameashiria mwezi aliozaliwa Baba wa Taifa, yaani mwezi wanne, na waliokimbia kilometa 22 ikiashiria mwaka aliozaliwa Baba wa Taifa.

Mhe. Kaegele ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kutengeneza barabara inayotumika kwa mbio hizo na kufafanua kuwa kuboreka kwa barabara hiyo kumefungua njia kwa watalii wengi kuja katika Hifadhi ya Serengeti.

“Niwaombe wakuu wa wilaya wa mikoa inayozunguka ziwa Victoria kuendeleza utalii wa fukwe, pia utalii wa madini na utamaduni kwa kutumia makabila yetu”amefafanua Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dkt. Thereza Mugobi wakati akitoa salam kwa niaba ya wakurugenzi wa Wizara.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Makumbusho ya Taifa nchini Dkt. Oswald Masebo amesema kwa kuendelea kuthamini mchango wa Baba wa taifa Taasisi yake itachangia madawati 50 kwenye shule aliyosoma Mwalimu.

Aidha ametoa rai kwa wadau wengine kuiga mfano wa makaumbusho ya Taifa ya kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa ambapo kwa upande wake Mwakilishi wa familia ya Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere amesisitiza kuwa familia inafarijika kuona kuwa serikali na wadau mbalimbali wameendelea kuenzi historia ya Baba wa Taifa.

Akitoa historia ya marathoni hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ambayo ndiyo mratibu mkuu wa tukio hilo kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utaliii, Dkt. Noel Luoga amesema mbio hizo zimeendelea kuboreka na kuwa amefafanua kwamba kwa mwaka huu zaidi ya washiriki 6000 na zaidi ya wakimbiaji 500 wamehudhuria katika mashindano haya. Pia imehusisha makundi maalum yaani wakimbiaji wenye mahitaji maalum na watoto.

Mkurugenzi wa Idara ya Malikale Dkt Kristowaja Ntandu ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu amesema kila nchi duniani ina utaratibu wake wa kuwaenzi waasisi wa mataifa yao, hivyo Wizara inatekeleza mpango wa miaka 10 wa kuhifadhi Historia ya Mwl Nyerere hivyo mbio hizo ni sehemu ya maadhimisho hayo huku zikiwa kama zao jipya la Utalii linalotangaza vivutio vya Utamaduni na urithi viliivyopo Mkoa wa Mara na mikoa jirani.

Marathoni ya mwaka huu imepambwa na matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na washiriki kutembelea kaburi la Baba wa Taifa na makumbusho, kupanda miti 101 ikiwa ni umri wa sasa wa Baba wa Taifa na Nyumba ya Baba wa Taifa. Pia mechi ya kirafiki baina ya Mtuzu na Kitanga na Mchezo wa Bao
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages