Breaking

Wednesday, 27 September 2023

MKURUGENZI MKUU TEA AWATAKA WATUMISHI KUONGEZA TIJA KATIKA UTENDAJI.

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa bidi, ubunifu na kuongeza tija ili kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

Dkt. Kipesha ametoa kauli hiyo leo Mkoani Dar es Salaam katika ofisi ndogo za TEA mara baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Septemba 23, 2023 kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo.

Aidha, amewasisitiza watumishi wa Mamlaka hiyo kuwa, nia na matarajio ya Mhe. Rais ni kuona TEA ikitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria lakini pia kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala. Hayo yote yanawezekana endapo kila mtumishi ataongeza bidi, kujituma na kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yake.

‘‘Naamini kila mtumishi anajua kuwa kazi kubwa ya TEA ni kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato ili kusaidia jitihada za Serikali za kuboresha miundombinu ya Elimu hapa nchini, hivyo kila mmoja ni lazima aweke bidii na ubunifu kwenye hili eneo ili TEA ifikie malengo yake, amesema Dkt. Kipesha’’

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Miradi na Utafutaji Rasilimali Bw. Masozi Nyirenda akiongea kwa niaba ya watumishi amesema, Mhe. Rais amempeleka mtu sahihi TEA kwani anaijua taasisi vya kutosha na ana uzoefu kwenye uongozi hivyo ana amini kwamba ataleta mabadiliko chanya ndani ya Mamlaka hiyo.

Ameongeza kuwa, watumishi wako tayari kushirikiana nae kwenye kila hatua na kutembea nae katika safari ya kusimamia na kutekeleza Mpango Mkakati wa TEA wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2025/2026 pamoja na Ilani ya Chama kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa Umma.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages