Breaking

Monday, 25 September 2023

MHE. KAIRUKI ASISITIZA VYOMBO VYA HABARI KUTANGAZA UTALII DUNIANI


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amevitaka  Vyombo Vya Habari  kutangaza  vivutio vya  utalii  ili watalii wengi waweze kuvifahamu  na kuja  nchini hatimaye  kuinua  uchumi wa nchi yetu.

Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea Televisheni ya TBC  jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Kituo hicho kabla ya  kufanya kipindi maalum kwa ajili ya kutoa ujumbe maalum wa Tanzania katika maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani ambapo  kauli mbiu ya siku hiyo kwa mwaka huo ni Utalii na Uwekezaji  Unaojali  Mazingira.

Aidha, amelitaka Shirika la Utangazaji Tanzania TBC kupitia chaneli yake ya utalii ya “Safari Channel” kufanya tafiti za  kuboresha  matangazo vivutio vya utalii katika nchi mbalimbali duniani na kujifunza kwa nchi zenye teknolojia  ya juu ya utangazaji wa vivutio hivyo ili  iweze kutangaza  vivutio vya utalii duniani.


“Ninawataka mtoke mwende  duniani mkajifunze wenzetu wanaendeshaje  chaneli  za utalii  ili na sisi  tuweze  kuendesha kituo chetu  vizuri zaidi kiweze kutangaza  vivutio vyetu vya utalii  duniani na kutuletea wageni wengi zaidi” amefafanua Mhe. Kairuki

Amesema  dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa tunatangaza  vivutio vya utalii watu wengi waweze kufahamu hazina ya vivutio vya Tanzania tulivyonavyo  ili waweze  kuja  kutembelea na kuliingizia taifa  mapato zaidi.


Aidha, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini  kusimamia Sekta za Maliasili na Utalii na kumhakikishia kuwa  ataendelea  kushirikiana na menejimenti ya wizara yake  na wadau mbalimbali kutekeleza  maono ya Serikali na ya  Mhe. Rais kutangaza  utalii wa Tanzania.

Maazimisho ya Siku ya Utalii duniani yanafanyika  jijini Riadhi Saudi Arabia ambapo Tanzania  pia inashiriki.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages