Breaking

Friday, 22 September 2023

MASHINDANO YA TUZO ZA UBORA KITAIFA AWAMU YA NNE YAFUNGULIWA RASMI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limefungua Mashindano ya Tuzo za Kitaifa Awamu ya Nne kwa mwaka 2023 ikiwa lengo ni kuhamasisha ubunifu na uboreshaji wa bidhaa na huduma zinazotolewa nchini kupitia taratibu zilizowekwa chini ya miundombinu ya ubora.

Maombi ya ushiriki yanaanza leo ambapo yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya nakala ngumu au kwa kilektroniki kwenye ofisi za TBS iliyopo karibu au ofisi za ZBS zilizopo karibu na pia unaweza kuwasilisha kwa njia ya baruapepe ambayo ni qualityawards@tbs.go.tz na mwisho wa maombi ni Oktoba 20,2023.

Akizungumza wakati akifungua Mashindano hayo leo Septemba 22,2023 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Bw.Lazaro Msasalaga amesema wazalishaji na watoa huduma wanahitajika kujengewa au kujijengea utamaduni wa ubora na ushindani hapa nchini.

Amesema moja ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara ni kujenga utamaduni wa kuthamini ubora kwenye jamii yetu kwa kuanzisha tuzo za kitaifa za ubora.

Aidha amesema kuwa malengo ya kuanzishwa kwa tuzo hizo ni pamoja na kuwatambua na kuwapongeza watu binafsi waliotoa mchango mkubwa katika kuboresha miundombinu ya ubora au taasisi zinazofanya vizuri kwenye masuala ya ubora wakati wa utekelezaji wa shughuli zao za uzalishaji bidhaa au utoaji huduma.

"Matarajio yetu mashindano ya tuzo kwa msimu wa nne kwa mwaka 2023 ambapo tunayazindua leo yatapata hamasa kubwa kutoka kwa wadau wa ubora na hivyo kupelekea ushindani wenye tija". Amesema

Pamoja na hayo amesema maandalizi, usimamizi na tathmini ya tuzo hizi yanafanywa na kamati maalum ambayo inahusisha taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara ya Viwanda na Biashara, TPSF, TBS, ZBS, TCCIA, NQA, TANTRADE pamoja na taasisi nyingine.

Hata hivyo ameeleza kuwa miongoni mwa vigezo vinavyotumika kuwapata washindi ni pamoja na nini kinafanywa na taasisi husika au mtu binafsi kuongeza ubora wa bidhaa, huduma, ufanisi katika uzalishaji au utendaji kazi kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Gasper Kahungya amesema mashindano haya ni muhimu kwani yataongeza chachu ya ushindani kwenye soko hasa kwa wazalishaji wa bidhaa waliopo sekta binafsi.

Vilevile ameipongeza TBS kwa kuandaa mashindano hayo ambayo ni muhimu kwa sekta binafsi na nchi kwa ujumla hasa katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora zinazozalishwa hapa nchini.

Nae Mratibu wa Tuzo za Ubora TBS, Bw. Baraka Mbajije amesema mchakato wa namna ya kushiriki mashindano hayo ni kujaza form ambazo zinapatikana kwenye website ya TBS, TPSF pamoja na ZBS ambapo unajaza form na kusaini kwa kuzingatia maelezo kulingana na kila kundi la ushiriki.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Bw.Lazaro Msasalaga akizungumza na waandishi wa habari wakati akifungua Mashindano ya Tuzo za Ubora Kitaifa Awamu ya Nne 2023 leo Septemba 22,2023 katika Ofisi za Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam.

Mwakilishi kutoka Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Gasper Kahungya akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Tuzo za Ubora Kitaifa Awamu ya Nne 2023 leo Septemba 22,2023 katika Ofisi za Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam.Mratibu wa Tuzo za Ubora TBS, Bw. Baraka Mbajije akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Tuzo za Ubora Kitaifa Awamu ya Nne 2023 leo Septemba 22,2023 katika Ofisi za Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages