Breaking

Wednesday 6 September 2023

MAAFISA USTAWI WA JAMII FANYENI KAZI KWA WELEDI - DKT. BITEKO



Na Mwandishi wetu- Dodoma

Maafisa ustawi wa jamii nchini wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia Sera, Sheria na miongozo mbalimbali ya utoaji wa huduma za ustawi wa jamii ili kuwezesha utoaji wa huduma bora.

Hayo yameelezwa Septemba 6, 2023 na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii wa Serikali na wa Sekta binafsi uliolenga kuweka mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto za kada hiyo na kuleta ustawi wa wananchi.

’’ Wapokeeni wahanga wa matendo ya ukatili, migogoro ya ndoa na mirathi na wahitaji wote wa huduma za ustawi wa jamii kwa upendo na kuwasikiliza vizuri ili kubaini kiini cha matatizo wanayopitia na kuwasaidia. Kutokana na changamoto wanazopitia baadhi yao wanakuwa wameanza kuathirika na tatizo la afya ya akili hivyo ni jukumu lenu kuwahudumia kwa upendo na kuwaonesha utu’’, alisisitiza Dkt. Biteko

Akisisitiza kuhusu masula mbalimbali Dkt. Biteko amesema baadhi ya wamiliki wa Makao ya Watoto, Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo Mchana na Makazi ya Wazee kutumia makao na vituo hivyo kama vitega uchumi kwa lengo la kujinufaisha wenyewe, naelekeza Waziri mwenye dhamana kushirikiana na vyombo vya sheria ili kuwabaini wamiliki hao na kuwachukulia hatua za kisheria.

’’Natoa rai kwa watu wote na taasisi zinazotoa huduma za Ustawi wa Jamii katika vituo visivyosajiliwa, kuvisajili vituo hivyo ndani ya siku tisini kutoka leo. Baada ya hapo, ukaguzi wa kina utafanyika ili kuwabaini watakaoshindwa kutimiza vigezo vya kisheria ili wachukuliwe hatua,’’ alisisitiza Dkt. Biteko

Sanjari na hilo amewataka maafisa ustawi hao kuendelea kusuluhisha migogoro kupitia Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii na Ofisi za Ustawi wa Jamii ngazi za Halmashauri nchini. Nimefahamishwa kwamba katika kipindi cha Julai 2022 hadi Aprili 2023, jumla ya mashauri 28,773 yalipokelewa na kati ya hayo 22,844 yalifanyiwa usuluhishi katika Mabaraza ya Usuluhishi na Ofisi za Ustawi wa Jamii na 5,929 yalipewa rufaa kwenda mahamakani. Aidha, nimejulishwa kuwa migogoro ya ndoa ilipungua kwa 27% katika kipindi hicho kutokana na jitihada zinazoendelea kufanywa na wadau mbalimbali. Pamoja na matokeo hayo mazuri, nasisitiza zaidi kuendelea kusuluhisha migogoro ya ndoa na kuipatia ufumbuzi haraka ili kutoathiri zaidi familia na ustawi wa jamii yetu.

Aidha, Wizara kuendelea kuwatambua na kuwapatia huduma watoto walio katika mazingira hatarishi ikiwa ni pamoja na huduma za chakula, malazi, mavazi, elimu, matibabu na lishe. Nimefahamishwa kuwa jumla ya watoto 335,971 (Me 168,634, Ke 167,337) walio katika mazingira hatarishi wametambuliwa na kupatiwa huduma katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Aprili 2023. Miongoni mwa hao, watoto 26,000 waliotelekezwa, manusura wa vitendo vya ukatili, wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu na wanaoishi kwenye makao ya watoto wameunganishwa na familia zao ili kuwahakikishia malezi, matunzo na ulinzi.

Pia, Dkt. Biteko alisisitiza kuwa Mhe. Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewaelekeza maafisa Ustawi wa Jamii kote nchini, kuendelea kutoa elimu ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kwa jamii ili kupunguza au kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye makundi mbalimbali ya kijamii.

Kazi nyingine aliyowaagiza Maafisa hao ni kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto katika maeneo yetu hususan majumbani, shuleni, kwenye vyombo vya usafiri na mitandaoni ili kulinda haki na ustawi wa watoto wetu. Ukatili kwa watoto unaathiri ukuaji wa mtoto na kusababisha nguvu kazi dhaifu na isiyokuwa na tija ya kutosha katika Taifa.

Hali kadhalika, Maafisa Ustawi wa Jamii wametakiwa kuimarisha zaidi Kampeni zenye lengo la kuelimisha jamii kuhusu masuala ya ukatili kwani uelewa mpana wa jamii ndiyo utawezesha kukomeshwa kwa vitendo vya ukatili.

Kwa upande wa Viongozi wa dini zote na wazee wa mila wametakiwa kuendelea kukemea vikali matendo maovu katika jamii yetu na kufundisha maadili mema. Ni imani yangu kuwa endapo waumini wa dini mbalimbali watazingatia mafundisho ya dini zao ustawi wa jamii yetu utaimarika kwa kuwa na familia bora zenye watoto waliolelewa na kufundishwa maadili mema.

Wazazi na walezi wametakiwa kuzingatia kikamilifu wajibu wao kulinda na kutunza familia zao. Na hapa, nakemea tabia ya baadhi ya wanaume ya kutelekeza familia zao na wengine kutowajibika kutunza watoto waliowazaa wenyewe. Napenda kutumia nafasi hii kuwaasa wanaume kuwa wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha familia zao zinakuwa salama ikiwa ni pamoja na kuzipatia mahitaji ya kila siku na kuziongoza vema.

Mkutano huu leo utaenda sambamba na Uzinduzi wa kuazimisha Miaka 50 ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Uzinduzi wa Wiki ya Ustawi wa Jamii pamoja na Uzinduzi wa Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji, Usimamizi na Uratibu wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa 2023; Mwongozo wa Mafunzo ya Uwiano wa Kijinsia na Ujumuishwaji Jamii katika Huduma za Ustawi wa Jamii 2022; na Kiongozi cha Taifa cha Uelimishaji wa Huduma za Ustawi wa Jamii na Majukumu ya Viongozi;
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages