Na Mwandishi Wetu ,
TAASISI ya Mama Ongea na Mwanao imesema inatarajia kuanza awamu ya pili ya kampeni ya Samia nivishe kiatu kwa kugawa viatu kwa wanafunzi wa shule zilizopo katika wilaya zote za Mkoa wa Lindi na Mtwara.
Imesisitiza katika kufanikisha kampeni hiyo imejipanga kuhakikisha wanashirikiana vizuri na Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumfikia kila Mtanzania wa kijijini na kumpatia kiatu kama sehemu ya kumuongezea hamu ya kupenda shule.
Akizungumza Septemba 14,2023 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steve Mengele maarufu Steve Nyerere amesema hakuna sare ngumu kupatikana kwa mwanafunzi kama kiatu, hivyo wao wameamua kubeba jukumu hilo.
“Wanafunzi wa mjini wao wanavaa tu la kuchumpa la kupalama, hivyo tutakwenda katika shule zote na tutahakikisha wanafunzi wanapata viatu, wanapata daftari.Lakini tutakuwa tunazungumza na walimu maana yake tunaweza kuwa tunawapa viatu na kila kitu lakini walimu hawaingii madarasani.
“Kwa hiyo na sisi tutashirikiana kuwambiaa walimu tunataka taifa endelevu lenye amani na utulivu kama Tanzania tukose vijana wenye elimu kutoka mjini na kutoka vijijini.Tunafahamu Elimu yetu ni bure na kama elimu ni bure lazima tuwajenge watoto kisaikolojia.
“Na kinachotakiwa ni kumuwezesha mtoto kupenda shule kwani anaweza akawa na daktari lakini hana kiatu.Katika sare sare ya shule ngumu ni kiatu , bukta unaweza kupata lakini kiatu ndio adimu sana katika shule zetu, unaweza kukuta mtoto hajavaa kiatu ana miaka mitano
“Wewe toto lako kila likirudi shule huku mjini halirudi na kile kiatu linaondoka na kipya.Sasa tunajiuliza tumewaandaliwa mazingira gani ya watoto kupenda shule?Hivyo tunaweza kumuandaa mtoto kwa kitu kidogo tu nacho ni kiatu,”amesema Stive Nyerere.
Amefafanua kuwa miaka ya nyuma kidogo walikuwa wanafunzi wanapewa madaftari bure na kumfanya mtoto kuwa na hamu na shule.
Akifafanua zaidi kuhusu kampeni ya kugawa viatu Stive Nyerere amesema walianza kampeni ya Samia Nivishe Kiatu kwa kwenda shule za vijijini.
“Kule vijijini ndiko tunawakuta watu wa nguvu kazi leo mimi nikiwambia kitu hamuwezi amini watu wanaotoka vijijini ndio wanakuja hapa wanakuwa matajiri wanapata vyeo sisi tupo tupo tu.
”Sisi ndio tunakuwa mdananda wao lakini mtu katoka kijijini ndio anakuwa tajiri, anapata vyeo, sisi ambao tuko mjini ndio tunajichukulia poa kawaida kwasababu hatuna kasi ya kutafuta maisha.
Tunakazi ya kutafuta umbea, tuna kazi ya kutafuta huyu anapata wapi hela, tuna kazi ya kutafuta kunyong’onyesha mtu lakini yule anayetoka kijijini anapata kasi ya kuhangaika na baadae sisi ndio tunaanza kumsalimia na kumuita mheshimiwa.
“Sasa tumewajengea uwezo gani?Tumeona twende tukawavishe watoto viatu na viatu vile humpi mwalimu mkuu .Ukifanya hivyo utakuta familia nzima inabadili tu ,watoto wa mwalimu mkuu anang’aa hatari.”
Amesema hivyo wameamua unapofika shule inapigwa kengelengele pale watoto wanapata viatu na mtoto anaondoka na kiatu chake kwenda nacho nyumbani .
“Hii tafsiri yake nini, inamfanya mtoto awe na hamu na shule .Unajua unaweza kuwa huna akili lakini unahamu na shule unakipenda kile kitu lakini mazingira unayoishi na kukutana nayo, unajua kule kijijini kuna kitu kinaitwa mbigili
“Ukichomwa mbigili sita huwezi kumsikiliza mwalimu ,wee kazi yako unawaza namna gani unatoa miba kwenye miguu. Hivyo Katiba yetu mpya tunakwenda kuvisha watoto viatu na tunapowavisha viatu watakuwa na hamu ya kupenda shule.
“Naa badae tunakwenda kujenga kizazi chenye tija , kizazi kinachopenda elimu , kizazi ambacho kitatuvusha na kulinda heshima ya taifa lao.Hatuwezi tukakubaliana kila mmoja apende , wengine watachukia, wengine watanuna, wengine watabinua midomo lakini sisi tunaenda kuwapa wale wengi viatu.”
Steve Nyerere amesema baada ya hapo watarudi kugawa daftari na huko mbeleni wanaweza kugawa na mabegi .Hivyo kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo watakuwa Lindi na baada ya hapo wataenda Mtwara, Ruvuma na kisha Dar es Salaam.
Amefafanua baada ya hapo watakwenda Mwanza,Mara na kurejea tena Dar es Salaam huku taasisi ikieleza tayari imegawa viatu 2000 katika wilaya ya Kibiti mkoani Pwani pamoja na Mkoa wa Tabora katika wilaya zake zote.