Breaking

Saturday, 9 September 2023

KAMATI YA BUNGE YA NISHATI YATEMBELEA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MTERA







Na Mwandishi Wetu, Iringa

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini leo imetembelea bwawa la Mtera ambalo ni miongoni mwa mabwawa yanayozalisha umeme nchini, kujionea namma umeme unavyozalishwa kwa njia ya maji na kuona maendeleo ya jumla ya umeme unavyozalishwa kwenye bwawa hilo

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Ussi Salum Pondeza amesema kuwa wananchi wengi wamekuwa na dhana ya kuamini kuwa TANESCO inafungulia maji bila utaratibu na hivyo kusababisha upungufu wa maji ya kuzalisha umeme Jambo ambalo si kweli kwani upo utaratibu maalumu unafuatwa kwa kushirikisha wadau wote.

Aidha Mhe. Ussi alisema wamejiridhisha na hali ya uzalishaji wa umeme kwenye bwawa la Mtera, na wamekuta mashine zote mbili zina uwezo wa kuzalisha megawati 72 huku kila moja ikizalisha megawati 38.

"Tumeridhika na uzalishaji licha ya kuwa kina cha maji kimepungua kutokana na kuchelewa kwa mvua ambazo zinajaza bwawa la Mtera na hivyo kusaidia uzalishaji pia kwenye mitambo ya Kidatu.

Amekemea upotoshaji huo na kuwaomba wananchi kutoamini taarifa hizo kwani TANESCO Ina vyanzo vingi vya uzalishaji umeme na kuwahakikishia wananchi kuendele kupata huduma hiyo kwa viwango vya juu

Kwa upande wake Mkurugenzi wa uzalishaji umeme kutoka TANESCO Mha. Pakaya Mtamakaya amesema Lengo la ziara ya kamati ya Bunge ni kujionea hali halisi ya uzalishaji umeme kwenye vyanzo vya maji vya Mtera, Kidatu, na kihansi na kujipanga iwapo mvua za kiwango cha juu zitanyesha kama ilivyotangazwa na mamlaka ya hali ya hewa hivi karibuni.

Alisema wanahakikisha umeme unaendelea kupatikana licha ya bwawa hilo kupungua kiwango chake cha maji kutokana na uhaba wa mvua.

" Kawaida huwa tunapata mvua Mara mbili kwa msimu na iwapo msimu ukichelewa husababisha uhaba wa maji, lakini hauathiri upatikanaji wa umeme kwani kuna vyanzo mbadala vya uzalishaji, alisema Pakaya.

Bwawa la Mtera ni miongoni mwa mabwawa kongwe yaliyojengwa baada ya uhuru na lina uwezo wa kuzalisha megawati 80.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages