Breaking

Wednesday, 20 September 2023

FILAMU TISA KUONESHWA MSIMU WA KWANZA TAMASHA LA SAUTI ZETU

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Jumla ya filamu tisa zikijumuisha filamu fupi na ndefu kutoka nchini Tanzania, Kenya na Afrika Kusini zinatarajiwa kuoneshwa katika msimu wa Kwanza wa Tamasha la Sauti Zetu ambalo linatarajia kufanyika katika Kituo cha Sanaa cha Little Theatre na maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam na Pwani kuanzia Oktoba 13 mpaka 15,2023.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 20,2023 Jijini Dar es Salaam, Afisa Mawasiliano kwa Umma MEDEA Tanzania, Bi. Justina Onguto amesema tamasha hilo linalenga kuleta jamii pamoja hususan vijana kusikia na kutazama hadithi zilizotungwa na kuzalishwa na waafrika zenye maudhui yanayochochea utawala bora, uhuru wa kujieleza na usawa wa kijinsia.

Amesema Juni 30 walifungua rasmi dirisha kwa ajili ya wazalishaji wa filamu kuwasilisha filamu zao na mchakato unatarajiwa kufungwa rasmi terehe 25 Septemba.

"Mpaka sasa tumefanikiwa kupokea filamu zaidi ya mia moja na majaji wetu wamekwisha anza mchakato wa kuzipigia kura na siku za hivi karibuni tutawataarifu kupitia mitandao yetu ya kijamii pamoja na tovuti ya filamu zilizochaguliwa msimu huu". Amesema

Amesema tamasha hilo litaambatana na shughuli nyingine ikiwemo kuwajengea uwezo wazalishaji wa filamu 15 kutoka maeneo tofauti nchini Tanzania.

"Mafunzo haya yatakuwa ni ya siku mbili yakidhamiria kuongeza ujuzi na maarifa kwa wazalishaji wetu wa filamu katika uandishi wa miswada, masoko na ukisanyani wa rasilimali za kuzalisha kazi ili kuongeza ubora wa filamu zetu na kusimulia hadithi zinazogusa maisha yetu, ndio maana tunasema "Hadithi Zetu, Sauti zetu".

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Filamu kutoka Bodi ya Filamu Tanzania , Bw. Emmanuel Ndumukwa amesema uandaaji wa matamasha kama hayo yanasaidia kuboresha kazi za kitanzania ziweze kuwa na ubora na kuwafaidisha wanaozifanya.

Amesema kupitia maonesho haya kwenye maeneo ya wazi, wengi watayatazama na kupenda kuangalia kazi za kwao.

Pamoja na hayo amewataka wadau wa filamu nchini kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha hilo kwaajili ya kuunga mkono juhudi za vijana wenzao.
Afisa Mawasiliano kwa Umma MEDEA Tanzania, Bi. Justina Onguto akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 20,2023 Jijini Dar es Salaam kuelekea msimu wa Kwanza wa Tamasha la Sauti Zetu ambalo linatarajia kufanyika katika Kituo cha Sanaa cha Little Theatre na maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam na Pwani kuanzia Oktoba 13 mpaka 15,2023.
Mratibu wa Tamasha, Bw. Elias Maeda akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 20,2023 Jijini Dar es Salaam kuelekea msimu wa Kwanza wa Tamasha la Sauti Zetu ambalo linatarajia kufanyika katika Kituo cha Sanaa cha Little Theatre na maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam na Pwani kuanzia Oktoba 13 mpaka 15,2023.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Filamu kutoka Bodi ya Filamu Tanzania , Bw. Emmanuel Ndumukwa akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 20,2023 Jijini Dar es Salaam kuelekea msimu wa Kwanza wa Tamasha la Sauti Zetu ambalo linatarajia kufanyika katika Kituo cha Sanaa cha Little Theatre na maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam na Pwani kuanzia Oktoba 13 mpaka 15,2023.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages