Breaking

Monday, 4 September 2023

DKT. BITEKO ASISITIZA HUDUMA YA NISHATI KUWAFIKIA WANANCHI WOTE



Na Mwandishi Wetu 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Judith Kapinga wamepokelewa rasmi na Menejimenti na Watumishi wa Wizara ya Nishati katika Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dodoma baada ya kuapishwa na Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kushika nyadhifa hizo.

Akizungumza na Menejimenti na Watumishi hao tarehe 4 Septemba, 2023, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amemshukuru Rais, Dkt. Samia kwa kumuamini katika kuisimamia Sekta ya Nishati na ameahidi kuwa yeye pamoja na Naibu Waziri watafanya kazi kwa bidii na ufanisi ili kuitendea haki imani hiyo.

Dkt.Biteko ameeleza kuwa, kazi iliyo mbele ni kuhakikisha kuwa huduma ya nishati inawafikia wananchi wote na kwamba, pamoja kazi nzuri iliyofanyika ya kuimarisha Sekta ya Nishati, bado kuna nafasi ya kufanya kazi hiyo vizuri zaidi ili nishati ya uhakika ipatikane, na hiyo ndiyo azma na matarajio ya Mhe.Rais na wananchi kwa ujumla.

“Kama watu hawapati umeme, kama watu hawapati nishati wanayoihitaji, hata tukivaa suti za namna gani tunakuwa hatuna maana na tutakuwa na tunasemwa kila siku, kiu yangu ni kuona tunafanya kazi kwa viwango ili huduma ya nishati iwafikie wananchi wote.”amesisitiza Dkt.Biteko

Amempongeza aliyekuwa Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba kwa juhudi alizofanya kuendeleza Sekta na kuahidi kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati itaendelea ili kufanya nchi kuwa na nishati ya uhakika.

Dkt. Biteko ameshukuru kwa mapokezi mazuri aliyopata wakati akiwasili Wizara ya Nishati na ameeleza kuwa atafanya kazi kwa pamoja na watumishi wa Wizara ili kuiendeleza Sekta na amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa amani.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyompatia ili kuweza kuhudumia Sekta ya Nishati kama Mbunge aliyetoka katika kundi la vijana na ameahidi uchapakazi, weledi na ufanisi katika kazi zake.

Mhe. Kapinga ameeleza kufarijika kwake kwa kurudi katika Sekta ya Nishati kwani tayari alishaanza kuwa na uzoefu nayo wakati akihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Amemshukuru Mhe. Rais pia kwa kumwezesha kufanya kazi chini ya Mhe. Dkt. Doto Biteko kwani ana uzoefu katika uongozi na Sekta ya Nishati hivyo chini ya uongozi wake ataendelea kukua na kufanya kazi kwa ufanisi.

Ameahidi kutoa ushirikiano kwa Watumishi wa Wizara ya Nishati na pia amewaasa Watumishi hao kumpa ushirikiano ili kwa pamoja waweze kutekeleza majukumu yatakayoendeleza Sekta ya Nishati na kusisitiza kuwa heshima ya mtu ni kazi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amempongeza Dkt.Doto Biteko kwa kuteuliwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati pia amempongeza Mhe.Judith Kapinga kwa kuaminiwa na Rais kuwa Naibu Waziri wa Nishati.

Mhandisi Mramba, amewakaribisha viongozi hao katika Wizara ya Nishati, na kueleza kuwa Wafanyakazi watatoa ushirikiano kwa viongozi hao ili kuweza kutekeleza majukumu yao kazi kwa ufanisi mkubwa.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages