Breaking

Friday 22 September 2023

DAWASA YAPEWA MBINU KUIMARISHA UPATIKANAJI WA MAJI







Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuanza kufikiria namna nzuri ya kuzalisha umeme ili utumike kuboresha uzalishaji wa maji na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote kwa kipindi chote cha mwaka.

Amesema kuwa kupatikana kwa umeme kutasaidia kupunguza changamoto ya kukosekana kwa huduma ya majisafi pindi umeme unapokosekana, pia utasaidia kupunguza gharama kubwa inayotumika kulipia umeme unaotumika kuendesha mitambo ya kuzalisha maji pamoja na vituo vya kusukuma majisafi kwa wananchi.

Ameyasema hayo wakati wa siku ya pili ya ziara yake ya kutembelea na kukagua hali ya upatikanaji wa maji, ambapo ametembelea mradi wa maji Kigamboni ikiwemo kituo cha kusukuma maji pamoja na tenki la maji la lita milioni 15 uliotekelezwa na Serikali kupitia DAWASA.

Ameongeza kuwa Mamlaka inafanya kazi kubwa ya kuzalisha na kusambaza maji kwa wananchi, lakini ukosefu wa umeme wa uhakika unasababisha huduma isifike kwa wateja kama ilivyokusudiwa, pamoja na kuathiri mitambo inayotumika kuzalisha na kusukuma maji kwenye maeneo ya kihuduma.

"Leo nimetembelea maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maji Kigamboni kwa lengo la kufuatilia agizo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha mitaa 11 ya Kata ya Kigamboni inapata huduma ya majisafi kupitia mradi wa maji Kigamboni ili wananchi waweze kunufaika kama lilivyo lengo la Serikali, nimeona kazi kubwa iliyofanyika na inaleta matumaini kuwa maji yatafika maeneo yote." amesema Mhe. Chalamila.

Ameongeza kuwa kwa sasa uzalishaji wa maji kwa Dar es Salaam na Pwani ni lita milioni 590 kwa siku huku mahitaji yakiwa ni lita milioni 544 na ongezeko la uzalishaji huu ambao umechagizwa na uwepo wa visima virefu vya Kigamboni.

Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe Halima Bulembo ameipongeza Mamlaka kwa kazi kubwa ya utekelezaji mradi wa maji Kigamboni na kasi ya usambazaji miundombinu katika maeneo mengi pamoja na kubaini wananchi wa kuunganishiwa huduma.

Ameiomba Mamlaka kuongeza kasi ya kuunganisha wananchi kwenye mitaa yao ili waweze kuwa na furaha na kuona manufaa ya mradi huu.

Akijibu hoja ya Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu alieleza kupokea agizo la Mhe Mkuu wa Mkoa la kufikiria kutengeneza umeme kwa matumizi ya maji na kuahidi kama Mamlaka watalifanyia kazi.

Amesema kuwa kwa lengo la kuboresha huduma, mojawapo ya jitihada kubwa zinazofanywa na Mamlaka ni pamoja na kuzalisha umeme kupitia mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda ambao zitapatikana Megawati 20 ambazo zitaingizwa katika gridi ya Taifa.

Mbali na hapo, kwa mwaka huu wa fedha Mamlaka imetenga shilingi bilioni 55 kwa ajiii ya kusambaza maji kwa wananchi kwenye maeneo yote ya huduma.

"Pia Mamlaka imeanza kazi kubwa ya kuchimba visima virefu 9 eneo la Kimbiji kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maji kwa lengo kuu la kuongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani," amesema Ndugu Kingu.


Mradi wa maji Kigamboni umetekelezwa na DAWASA kwa gharama ya bilioni 25 na unalenga kunufaisha wakazi 450,000 wa Kigamboni na maeneo ya pembezoni.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages