Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani kushuhudia tukio la kihistoria la kuhama kwa Wanyama (Nyumbu) kwenye eneo la Kogatende katika mbuga ya Serengeti.
Katika tukio hilo lililodumu kwa zaidi ya masaa mawili Nyumbu zaidi ya elfu kumi wakisindikizwa na mamia ya pundamilia na baadhi ya Tembo wamevuka mto Masai Mara kutoka upande wa Kenya kuja Tanzania.
Pamoja na Waziri wa Utalii Mhe. Mohammed Mchengerwa, pia walikuwepo viongozi wengine ambazo ni Naibu wake, Mary Masanja, Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu Benedict Wakulyamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe Timotheo Mnzava ambae aliongoza baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo kushuhudia tukio hilo la kihistoria na kubaki wakishangazwa na maajabu hayo.
“Ndio tumeanza kutekeleza mikakati kabambe ya kuutangaza utalii wetu. Tukio hili ni la kihistoria na huwezi kulikuta popote duniani; ujio wetu hapa ni kulipia tukio hili heshima na kulitangaza zaidi duniani,” alisema Waziri Mchengerwa.
Akitoa hotuba mara baada ya kushuhudia makundi makubwa ya nyumbu kuvuka mto Mara Waziri Mchengera amesema sekta ya utalii ni miongoni mwa nguzo muhimu katika uchumi na maendeleo ya nchi ya kutokana na mchango wake katika pato la Taifa,
Amesema sekta hiyo huchangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la Taifa (GDP) na takriban ajira milioni 1.5 za moja kwa moja na ambazo si za moja kwa moja na amefafanua kwamba Sekta ya Utalii nchini imevunja rekodi mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ongezeko ambalo halijawai kutokea.
Amesema takwimu zinaonesha kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 Tanzania ilipata jumla ya watalii 1,638,850 walioingizia taifa jumla ya shilingi bilioni 522.7 ikilinganishwa na watalii 1,123,130 walioingizia taifa shilingi bilioni 290.4 mwaka wa fedha 2021/2022.
Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 45.9 ya watalii na mapato asilimia 80, amesema na kuongeza kuwa lipo ongezeko kubwa la watalii na mapato kwa kipindi cha Januari hadi Juni, 2022/2023 ukilinganisha na kipindi kama hicho 2020/2021. Kutoka 575,397 na mapato ya shilingi bilioni 130,592,796,544 Januari hadi June, 2022 hadi kufikia watalii 759,327 na mapato shilingi bilioni 202,375,961,009 Januari hadi Juni, 2023.
Ameongeza kuwa Watalii wote waliokuja nchini Mwaka wa fedha 2022/2023 asilimia 37.6 walitoka nchi kumi za bara la Ulaya, Amerika na Asia ukilinganisha na asilimia 31 ya watalii waliofika nchini kutoka nchi hizo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022. Watalii kutoka Marekani (118,108) waliongoza mwaka wa fedha 2022/2023 wakati watalii kutoka Ufaransa (76,084) waliongoza kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Amefafanua kuwa ukuaji huu unatokana na juhudi za kutangaza Utalii kupitia Filamu ya Tanzania the Royal Tour iliyoasisiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na mikakati mbalimbali iliyowekwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo amesisitiza kuwa pamoja na mambo mengine, Mikakati hiyo imewezesha Tanzania kuchaguliwa na Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) kuwa Makamu wa Rais Baraza Kuu UNWTO Kimataifa, kuwa Mjumbe Kamati ya Utendaji UNWTO Kimataifa na kuwa Mjumbe wa Kikundikazi cha Wataalam (Brand Africa).
Tukio la kuhama kwa nyumbu katika Mfumo Ikolojia wa Serengeti hutokea kwa mwaka mzima ikijumuisha nyumbu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 1.5 wakiambatana na wanyamapori wengine wakiwemo Pundamilia takriban 400,000, Swala 200,000 na Wanyamapori wengine kutafuta malisho, maji na hali nzuri ya hewa. Wakati wa kuhama wanyamapori hawa hupitia maeneo mbalimali yenye vikwazo na fursa katika kukamilisha mzunguko wao.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timetheo Mnzava amesema; “Tumejionea maajabu leo na tunaipongeza Serikali na wahifadhi wetu kwa kuwalinda wanyama hawa mpaka leo tumejionea tukio hili la aina yake,”.