Breaking

Friday, 25 August 2023

WAZIRI MCHENGERWA AZINDUA AWAMU YA PILI YA KUHAMA NGORONGORO, AONYA WATAKAOHUJUMU ZOEZI


Na John Mapepele.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa ameonya mtu au kikundi chochote kitakachojitokeza kuhujumu zoezi linaloendelea la kuhama kwa hiari wananchi wanaoishi kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kupisha uhifadhi.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Agosti 24, 2023 wakati alipokuwa akizindua awamu ya pili ya zoezi la kuhama kwa hiari na kuziaga kaya 16 zilizokuwa zikiishi hifadhini na kutoa hundi za fedha kwa familia hizo.

Amefafanua kuwa zoezi la kuhama ni zoezi la hiari ambapo mtu mwenyewe bila kushinikizwa na mtu ana hiari ya kuondoka lakini asitokee mtu wa kuwarubuni na kuwadanganya watu walioamua kuhama kwa hiari yao kwa kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wanafanya jinai na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Serikali ina mkono mrefu na macho kila pembe ya nchi hii, niwahakikishie kuwa yeyote ambaye atathubutu kuhujumu jitihada za Serikali za kuwaletea maisha bora na uhifadhi wa raslimali za Taifa atakumbana na mkono wa Sheria”. Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Aidha, amesema dhamira ya Serikali ni kutaka wananchi wake wanapata haki zao za msingi za kuishi maisha bora na kupata huduma zote za kijamii kama elimu na afya bila kubughudhiwa na mtu.

Amesema Serikali inaendelea na zoezi la kuhamisha wakazi wa Ngorongoro kwa hiari kwenda katika eneo la Msomera na maeneo mengine hapa nchini ambapo Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Februari, 2022, ambapo amefafanua kuwa katika awamu ya kwanza iliyoishia mwezi Januari, 2023, jumla ya kaya 551 zenye watu 3,010 na mifugo 15,521 zimekwishahamia katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni na maeneo mengine.

Pia amesema katika awamu ya kwanza Serikali ilijenga nyumba 503, shule ya msingi, shule ya sekondari, kituo cha afya, miundombinu ya maji na umeme, majosho, barabara na kituo cha polisi.

Amesema awamu ya pili ya zoezi la kuhamisha wakazi wa Ngorongoro, Serikali imepanga kujenga nyumba 5,000 ambapo utekelezaji wa awamu ya pili unaanza rasmi Agosti 24,2023, na jumla ya kaya 16 zenye jumla ya watu 87 na mifugo 309 zinahamia katika Wilaya ya Karatu na Monduli.

Amewapongeza wananchi wote waliojitokeza kujiandikisha na kuhama kwa hiari kwenda katika maeneo mbalimbali na amehimiza wananchi wanaotaka kuhama kwa hiari wenyewe wajitokeze kujiandikisha ili wapate fursa ya kuhama kwenda katika maeneo mengine watakayopenda wenyewe na vilevile kwenda katika maeneo ya Msomera/Kitwai.

Amesema Serikali itaendelea kuwawezesha wananchi wote watakaojitokeza kuhama kwa hiari.

Akitoa taarifa ya zoezi hilo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Ngorongoro, Elibariki Bajuta amesema zoezi la kuhamisha kwa hiari kwenda Msomera ulianza Juni 16,2022 ambapo hadi kufikia Januari 18, 2023 jumla ya kaya 551 zenye 551 zenye watu3,010 na mifugo 15,321 zilikuwa zimehamia kijiji cha Msomera na maeneo mengine.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages