Breaking

Monday, 14 August 2023

WAZIRI MCHENGERWA AANIKA MAENDELEO MAKUBWA YA RAIS SAMIA, AHIMIZA UMOJA, AMANI


Na John Mapepele

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Mkoa wa Pwani na Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imewaletea wananchi maendeleo makubwa katika kipindi kifupi na kuwataka wanaCCM kote nchini kuyaeleza mafanikio hayo yaliyopatikana ili kuondoa upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu wenye nia mbaya ili washike dola.

Mhe. Mchengerwa ameyasema haya Agosti 13, 2023 Ikwiriri wilayani Rufiji wakati akimkaribisha Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwishehe Ramadhan Mlao kuwahutubia wana CCM kwenye kikao maalum cha kuwashukuru kwa kuwachagua viongozi wao katika uchaguzi uliopita.




Aidha, amesisitiza kuwa kwa sasa wanaCCM hawatakubali kuendelea kuona baadhi ya watu wanaendelea kukejeli maendeleo makubwa yaliyoletwa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Rais wetu anatufanyia kazi kubwa sana katika mkoa wetu wa Pwani na Tanzania kwa ujumla wake, Rufiji tulikuwa na ndoto tu, tulikuwa hatuna barabara lakini hadi sasa tayari ameshatuletea fedha zote ni jukumu sasa la Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na timu yake kusimamia ili kazi zote zikamilike kwa wakati.” Amefafanua Mhe. Mchengerwa




Akitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hiki kwa Wilaya ya Rufiji kuwa ni pamoja na kuanza matengenezo ya barabara kwa kiwango cha rami ambazo zilikuwa hazijawahi kutengenezwa tangu Tanzania kupata uhuru, ambazo ni barabara ya Nyamwage -Utete, barabara na daraja la Mbande na barabara ya Ikwiriri-Mkongo.

Mafanikio mengine ni kukamilika kwa miradi ya ujenzi wa shule, zahanati vituo vya afya na taa za barabarani ambapo amesisitiza kuwa havikuwepo katika nyakati zote zilizopita isipokuwa wakati wa sasa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan hivyo anapaswa aungwe mkono ili aendelee kuwaletea watanzania maendeleo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages