Breaking

Friday, 18 August 2023

WAZEE WA MILA SERENGETI WAGEUKIA TOHARA SALAMA

Mzee wa Kimila Wilaya ya Serengeti (aliyevaa kofia) akielezea hatua walizochukua kuondokana na tohara ya kimila kwa vijana. Mwingine ni Mratibu wa Tohara Wilaya ya Serengeti Dkt. Mary Yohana Kisiri.


Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Juhudi za kukabiliana na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI yanayotokana na wanaume kufanyiwa tohara za kimila katika Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara zinazidi kuzaa matunda baada ya Wazee wa Kimila kupata mwamko chanya juu ya tohara kinga ya kitabibu ambayo imekuwa ikitolewa katika vituo vya afya na katika jamii.


Matokeo hayo chanya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na nguvu ya Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani (PEPFAR), kupitia Kituo cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa cha nchini Marekani (CDC) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na Shirika la Amref Health Africa Tanzania ambalo linatekeleza huduma za kupambana na VVU/UKIMWI katika jamii kulingana na ushahidi wa kitafiti kwa makundi ya watu yaliyo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU ambapo pia limo kundi la wanaume wanaofanyiwa tohara za kimila.

Inaelezwa kuwa mbali na Wilaya ya Tarime, Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara pia inatajwa kuwa na idadi kubwa ya wazee wa kimila na mangariba ambao wamekuwa wakifanya tohara za kimila kwa vijana lakini sasa wameanza kubadilika kwa kuachana na utamaduni huo wa tohara za kimila na kuhamasisha tohara kinga za kitabibu.

Akizungumza na Waandishi wa habari waliofanya ziara Mkoani Mara ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya PEPFAR tangu ilipoanzishwa mwaka 2003, Mmoja wa Wazee wa Kimila aliyejitambulisha kwa jina la John Marwa kutoka Nyamoko Wilaya ya Serengeti amesema hivi sasa wameikubali tohara kinga ya kitabibu.

“Amref Health Africa Tanzania ambao wanatekeleza Mradi wa Afya Kamilifu wametoa wamefika katika jamii na kutoa elimu ya tohara kinga ya kitabibu, elimu hii imetusaidia kubadilika. Lakini pia wamekuwa wakitupatia vifaa vya kisasa vya kufanyia tohara salama kwa vijana”,amesema Mzee Marwa.

Amesema licha ya kutumia dawa za kienyeji kuzuia damu nyingi zisitoke wakati wa tohara, vijana wamekuwa wakitokwa damu nyingi, hivyo kusababisha baadhi ya kuzimia na wakati mwingine kusababisha kifo na wengine kupata maambukizi ya VVU kutokana na kutumia kifaa kimoja cha kufanyia tohara ya kimila.

“Wakati tunafanya tohara za kimila tulikuwa tunatumia kisu kimoja, vijana walikuwa wanatokwa damu nyingi. Kipindi cha nyuma kijana wa kiume akifanyiwa tohara akavuja damu nyingi akafariki, tulikuwa hatumziki, tulikuwa tunawatupa ili ukoo usipate laana”,ameeleza Mzee Marwa.

“Sasa hivi vijana wanaopata tohara hospitali/kwenye kituo cha afya hawatengwi kwenye jamii kama ilivyokuwa mwanzo ambapo kama kijana hajafanyiwa tohara ya kimila alikuwa anatengwa, anachekwa hali iliyosababisha baadhi ya vijana ili kuepuka kutengwa hata kama amefanyiwa tohara ya kitabibu alilazimika kufanyiwa tena tohara ya kimila. Sasa hivi hatutahiri mara ya pili, mambo ni shwari hivyo, waliofanyiwa tohara hospitalini na waliofanyiwa kimila wote ni sawa”,ameongeza Mzee huyo kutoka Serengeti.
Mhamasishaji wa masuala ya tohara salama kutoka kwa Wazee wa Kimila wilaya Serengeti, Charles Mwita.

Kwa upande wake, Mhamasishaji wa masuala ya tohara salama kutoka kwa Wazee wa Kimila wilaya Serengeti, Charles Mwita amesema wanaendelea kutoa elimu na uhamasishaji wa tohara kinga ya kitabibu kwa wazee wa kimila ili kukabiliana na maambukizi ya VVU kwani vifaa vinavyotumika katika tohara ya kimila vinachangia maambukizi ya VVU.


“Kupitia PEPFAR tumewapa elimu na kuwaaminisha wazee kuhusu tohara salama. Hata tohara za kimila zinazoendelea tunawapa vifaa vya kufanyia tohara salama. Kwa kweli Serengeti imebadilika, itaendelea kubadilika na hatimaye jamii itaachana kabisa na tohara za kimila”,ameeleza Mwita.


“Tohara ya kimila ni hatari, hebu fikiria kisu kimoja kilikuwa kinatumika kuwafanyia tohara vijana 1000, damu nyingi zinatoka hapo tutakwepaje maambukizi ya VVU?...Sasa hivi jamii imebadilika sana, imefikia hatua hadi baadhi ya vijana waliofanyiwa tohara ya kinga ya kitabibu hospitalini wanafanyiwa sherehe kama walivyokuwa wanafanyiwa sherehe vijana waliofanyiwa tohara ya kimila kwenye jamii. Haya ni mafanikio makubwa tunayoweza kujivunia kupitia PEPFAR”,ameongeza Mwita.

Naye Mratibu wa Tohara Wilaya ya Serengeti Dkt. Mary Yohana Kisiri amesema wakati wanaanzisha huduma ya tohara ya kitabibu mwitikio ulikuwa mdogo lakini sasa mwitikio ni mkubwa ambapo licha ya wanaume kupata huduma ya tohara kinga kwenye jamii kupitia Mkoba, wengi wamekuwa wakifika kwenye vituo vya afya kupata huduma hiyo bure.
Mratibu wa Tohara Wilaya ya Serengeti Dkt. Mary Yohana Kisiri.

“Tunaishukuru Serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuleta huduma ya tohara bure kwa wanaume katika vituo vya afya na hospitali. Mwitikio ni mzuri, kwa mfano tangu mwaka 2021 mpaka sasa jumla ya vijana 7832 wamepatiwa huduma ya tohara kinga katika wilaya ya Serengeti”,anaeleza Dkt. Kisiri.

“Mwanzo vijana waliopata tohara kinga ya kitabibu walikuwa wanapata changamoto ya kunyanyapaliwa, lakini sasa unyanyapaa umepungua. Wazee wa kimila wanatoa ushirikiano mkubwa , hata ikitokea kijana aliyefanyiwa tohara ya kimila akapata changamoto wanashiriki kumleta hospitali. Tunashukuru wazee wa mila pia wanawaleta vijana kupata tohara salama”,amesema Dkt. Kisiri.

Kwa upande wake, Mratibu wa UKIMWI wilaya ya Serengeti, Dkt. Damas Ngwegwe anaishukuru Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania kwa hatua walizochukua kukabiliana na maambukizi ya VVU katika jamii ikiwa ni pamoja na kutoa huduma ya tohara kinga kwa wanaume.

“Tumekuwa tukitoa elimu ya kubadili jamii, mwitikio ni mzuri. Jamii imekuwa na utaratibu wa kufanya tohara za kimila, vijana walikuwa wakifanyiwa tohara ya kimila wanafanyiwa sherehe na sisi tukaanzisha sherehe kwa vijana waliofanyiwa tohara kinga ya kitabibu/tohara salama. Mambo yanaendelea kuwa mazuri”,amesema Dkt. Ngwegwe.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu, kupitia PEPFAR mpaka sasa wamefanikiwa kuwafanyia tohara kinga ya kitabibu wanaume wapatao 63,000 mkoani humo ambapo hayo yote yanatokana na uhamasishaji wa tohara ya kitabibu inayotolewa bure kwa wanaume ikiwa ni juhudi za kukabiliana na maambukizi ya VVU.

Mhamasishaji wa masuala ya tohara salama kutoka kwa Wazee wa Kimila wilaya Serengeti, Charles Mwita akielezea kuhusu tohara salama kwa wanaume
Mratibu wa UKIMWI wilaya ya Serengeti, Dkt. Damas Ngwegwe akizungumzia masuala ya tohara kinga za kitabibu
Mratibu wa UKIMWI wilaya ya Serengeti, Dkt. Damas Ngwegwe akizungumzia masuala ya tohara kinga za kitabibu
Mratibu wa Tohara Wilaya ya Serengeti Dkt. Mary Yohana Kisiri akielezea kuhusu huduma ya tohara kinga/tohara salama kwa wanaume
Bango likionesha huduma zinazotolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara
Muonekano wa mbele Hospitali ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages