Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI wa shule ya Brilliant Dk. Jasson Rweikiza, amesema hakuna mwanafunzi wa shule hiyo atakayefukuzwa kwa kukosa ada baada ya kufiwa na mzazi wake au mlezi aliyekuwa akimlipia ada.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo ambalo mgeni rasmi alikuwa Meya wa Ubungo jijini Dar es Salaam.
Alisema wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Uviko wazazi 42 wa wanafunzi wa shule zake walikufa lakini hakuna hata mwanafunzi mmoja aliyefukuzwa shule kwa kukosa ada.
“ Mwaka 2021 kwenye shule zetu tulipoteza wazazi 42 kukawa na kilo kikubwa kwa wanafunzi tukatafuta namna na tukaamua kwamba hakuna mwanafunzi wa shule ya Brilliant au St Anne Marie Academy ambaye atafukuzwa shule kwa kukosa ada baada ya kufiwa na mzazi au mlezi wake,” alisema Dk. Rweikiza ambaye ni Mbunge wa CCM, Bukoba vijijini.
Alisema walimu wa shule hiyo wamejitahidi kuwaandaa kitaaluma na kinidhamu na wengi wameahidi kwamba watafaulu kwa daraja la kwanza na daraja la pili pekeee.
Alisema kazi kubwa ya shule ni kufundisha na kufaulisha wanafunzi kwa hiyo walimu wa shule hiyo wamekuwa wakifanyakazi usiku na mchana kuhakikisha wanafunzi wote wanafaulu kwa kiwango cha kuridhisha.
Alisema wale wataopenda kuendelea na kidato cha tano katika shule ya St Anne Marie Academy watapatiwa punguzo la ada kwa asimilia 15.
“Siyo kwamba naipigia debe St Anne Marie wanafunzi tunao wengi na tumekuwa tukifaulisha kwa alama za juu mfano matokeo ya kidato cha sita mwaka jana daraja la kwanza walikuwa 64, daraja la pili 119 na daraja la III wanafunzi 49,” alisema
Alisema kuanzia mwaka 2024 mtaala wa elimu utabadilika sana ambapo shule ya msingi itaishia darasa la sita badala ya darasa la saba.
Alisema wanafunzi wote wanaomaliza elimu ya msingi wataendelea mpaka kidato cha nne na watakuwa na uwezo wa kuchagua masomo badala ya kusoma masomo tisa au kumi watakuwa na uwezo wa kuchangua.
“Mwanafunzi atakuwa na uwezo wa kuchagua masomo manne na ya ufundi aendelee nayo ili anapomaliza kidato cha nne aajiriwe moja kwa moja au ajiajiri mwenyewe au asome masomo yote kumi aende kidato cha tano na chuo kikuu,” alisema
Alisema shule zake zimeshafanya maandalizi kwa kuwaajiri walimu wa kilimo, uvuvi, ufundi ili vijana waandaliwe kuendana na mtaala mpya wa serikali ambao utaanza kutumika mwakani.
Alisema wamejitahidi kuwafundisha na kuwahimiza wanafunzi wa shule hiyo wawe na nidhamu na juhudi ya kusoma kwani hakuna siri ya mafanikio kitaaluma zaidi ya kusoma.
“Nimewaahidi zawadi mbalimbali watakaofanya vizuri na nimeona niliseme hili mbele ya wazazi ili kuonyesha kwamba sisi tuko makini na zawadi hizi tunatoa kila mwaka,” alisema
Dk. Rweikiza alisema wanafunzi wote watakaofaulu kwa daraja la kwanza na la pili watapelekwa kutalii bungeni Dodoma na mbuga ya Mikumi iliyoko mkoani Morogoro ili wafurahie matunda ya juhudi zao.
Alisema wanafunzi watakaofaulu kwa daraja la kwanza pointi 16-17 watapewa zawadi ya simu janja kwamba wale watakaopata daraja la kwanza pointi 11-16 watapewa zawadi ya simu janja na shilingi 100,000.
Alisema wanafunzi watakaopata daraja la kwanza kuanzia pointi 10 watapata zawadi ya simu janja na shilingi 200,000 wakati wale watakaopata daraja la kwanza pointi tisa watapata zawadi ya simu janja na shilingi 500,000.
Aidha, Dk. Rweikiza alisema watakaopata daraja la kwanza point inane watapata simu janja na shilingi 1,000,000 na watakaopata daraja la kwanza pointi saba watapata simu janja shilingi 2,000,000 na kwamba atakapotokea wa kwanza kitaifa atapata zawadi ya shilingi 4,000,000.
“Nimesema atakayekuwa wa kwanza kitaifa na siyo ajabu kwasababu mwaka juzi pale st Anne Marie mwanafunzi wa kwanza kitaifa alitokea pale kwa hiyo someni kwa bidii zawadi zipo kwaajili yenu tutatoa hadi iphone macho matatu, someni muda umebaki mdogo ” aliahidi Dk. Rweikiza
Meya wa Ubungo, Jafary Juma alishangazwa na vipaji vya wanafunzi wa shule hiyo na kumpongeza Dk. Rweikiza kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya kwenye elimu.
Meya alisema uwekezaji huo umekuwa mchango mkubwa kwa serikali kwani amesaidia kuondoa ujinga kwa kutoa elimu kwa mamia ya watanzania wanaosoma kwenye shule zake.
“Nimefurahishwa na namna wanafunzi wa shule hii wanavyomudu lugha za kigeni kama Kifaransa na Kiingereza, wanazungumza kwa ufasaha kana kwamba wanazungumza Kiswahili, walimu na uongozi mnastahili pongezi sana, “ alisema Jafary.
Meya wa Ubungo, Jafary Juma akivishwa skafu wakati akikaribishwa kwenye mahafali ya 13 ya kidato cha nne ya shule ya Brilliant ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam ambapo wanafunzi 129 wanatarajia kuhitimu kidato cha nne Novemba mwaka huu. Kulia kabisa ni Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk. Jasson Rweikiza
Meya wa Ubungo, Jafary Juma akiwasili kwenye mahafali ya 13 ya kidato cha nne ya shule ya Brilliant ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam ambapo wanafunzi 129 wanatarajia kuhitimu kidato cha nne Novemba mwaka huu. Katikati ni Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk. Jasson Rweikiza
Wahitimu watarajiwa wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Brilliant ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam wakiingiwa kwa mbwembwe kwenye mahafali hayo yaliyofanyika shuleni hapo mwishoni mwa wiki
Wahitimu watarajiwa wa kike wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Brilliant ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam wakiingiwa kwa mbwembwe kwenye mahafali hayo yaliyofanyika shuleni hapo mwishoni mwa wiki
Wahitimu watarajiwa wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Brilliant ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam wakiserebuka kwenye mahafali hayo yaliyofanyika shuleni hapo mwishoni mwa wiki