Breaking

Sunday, 20 August 2023

TWIGA MINERALS CORPORATION KINARA TUZO YA UTOAJI BORA WA GAWIO KWA SERIKALI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Meneja wa Barrick Nchini, Melkiory Ngido (katikati) na Mjumbe wa Bodi wa Twiga Minerals na makampuni ya Barrick nchini, Casmir Kyuki (kulia) cheti cha mlipa gawio kubwa Serikalini wakati wa kikao kazi cha Wenyeviti na Watendaji wa taasisi za umma jijini Arusha
Kampuni ya Twiga Minerals Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Corporation, imeshinda tuzo bora ya utoaji gawio kwa Serikali katika kipengele cha Kampuni zenye ubia na Serikali.

Tuzo ya ushindi kwa kampuni hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki jijini Arusha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye ufunguzi wa kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu na Taasisi za Umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Umma.


Akizitaja kampuni zilizofanya vizuri katika kipengele hicho, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amesema kuwa kampuni ya Twiga Minerals, imefanya vizuri katika kipengele hicho kwa kutoa gawio kwa Serikali ya kiasi cha shilingi bilioni 84 Mwaka wa Fedha 2022/23.

Migodi iliyopo chini ya kampuni ya Twiga Minerals ni pamoja na North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi.

Mwezi Januari, 2023 wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Meneja wa kampuni ya Twiga nchini, Melkiory Ngido, alisema mwaka 2020 kampuni hiyo ilitoa gawio kwa Serikali kiasi cha Dola za Marekani milioni 250 huku kipindi cha mwaka 2017 hadi 2022 kiasi cha shilingi bilioni 24.3 kilitolewa kwa halmashauri kama tozo mbalimbali zinazotozwa katika maeneo yenye shughuli za migodi yake.


" Kampuni ya Twiga imepanga kuendeleza shughuli za utafiti ili kuongeza uhai wa migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu na ni matazamio ya uhai wa mgodi wa Bulyanhulu ni kufika mwaka 2040 na North Mara kufika mwaka 2039," alisema Ngido katika kikao hicho.


Akiongea na waandishi wa habari nchini hivi karibuni, Rais na Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, alisema Kampuni ya Madini ya Twiga, ambayo ni ya ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Dahabu ya Barrick, imefufua tasnia ya madini ya dhahabu nchini kupitia ubia ambao unafaa kuwa mfano wa kuigwa kwa shughuli kama hizo, hususan katika nchi zinazoendelea.


Bristow alisema tangu kuanzishwa Kampuni ya Twiga kama ubia wa kugawana faida za kiuchumi kwa uwiano wa 50:50 ambao pia Serikali ya Tanzania inao umiliki wa hisa wa 16% katika kila mgodi uboreshaji wa migodi umeimarika na uendeshaji huu wa shughuli umefanikiwa sana kiasi kwamba, tangu Barrick inunue hisa kutoka kwa wanahisa wenye hisa chache, umechangia kiasi cha zaidi ya dola bilioni 2.8 katika uchumi wa Tanzania kupitia kodi, ushuru, magawio, mishahara na malipo kwa wazabuni wa ndani.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages